NIGERIA-MAREKANI-USALAMA

Nigeria yajikuta kwenye orodha nyeusi ya Marekani kwa kuzuia uhuru wa kidini

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari © Nigeria Presidency

Marekani imeiweka Nigeria kwenye orodha yake nyeusi ya nchi "zinatia wasiwasi zaidi" kwa suala la uhuru wa kidini, linalochukuliwa kuwa "la kwanza katika masuala ya uhuru" na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo.

Matangazo ya kibiashara

Marekani inasema uhuru wa kuabudu na kidini ni nguzo ya haki msingi za binadamu, kwa hiyo lazima iheshimishwe.

"Uungwaji mkono wa Marekani katika suala la uhuru wa kidini ni muhimu," Waziri wa Mambo ya Nje w Marekani Mike Pompeo ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

"Orodha nyeusi ya kila mwaka inaonyesha kwamba wakati uhuru wa kidini unatishiwa, tunachukua hatua," Mike Pompeo ameonya.

Nchi zingine zilizo kwenye orodha hiyo nyeusi ya Marekani ni zile zile kama mwaka 2019: Saudi Arabia, Burma, China, Korea Kaskazini, Eritrea, Iran, Pakistan, Tajikistan na Turkmenistan.

Mike Pompeo hakuelezea sababu za kuorodheshwa kwa Nigeria, ambayo tayari ilikuwa imewekwa "chini ya uangalizi" mnamo mwaka 2019.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni juu ya uhuru wa kidini duniani iliyochapishwa mwezi Juni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iligundua mvutano kati ya mamlaka na kundi la Kishia lenye itikadi kali la Shia Islamic Movement of Nigeria (IMN), ambapo maandamano yao hukandamizwa mara kwa mara.

Ripoti hiyo imebainisha kwamba marufuku ya kuanzisha dini hili mwaka jana ililaaniwa na Kanisa Katoliki nchini Nigeria, ambalo linaona kama tishio kwa uhuru wa kidini kwa ujumla.

Ripoti hiyo pia inataja kukamatwa kwa Waislamu baada ya kupatikana na hatia ya kula hadharani katika jimbo la Kano wakati wa mfungo wa Ramadhan.

Mike Pompeo, Mkristo mwaminifu wa Kiinjili, ameweka utetezi wa uhuru wa kidini kuwa kipaumbele chake katika masuala ya haki za binadamu, suala ambalo halitiliwa sana umuhimu na utawala wa Donald Trump.