DRC-SIASA-TSHISEKEDI-KABILA

DRC: Mvutano mkali kati ya wafuasi wa Tshisekedi na Kabila katika Bunge la Kitaifa

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ISSOUF SANOGO / AFP

Nchini DRC, wabunge wanaomuunga mkono rais Felix Tshisekedi na wengine kutoka upinzani wanataka kuangusha ofisi ya Bunge ambayo kufikia sasa inadhibitiwa na kambi ya Kabila.

Matangazo ya kibiashara

Makabiliano makali yameripotiwa kati ya kambi mbili katika makao makuu ya Bunge. Mvutano ulionekana kupungua Jumanne jioni.

Kwa siku ya pili mfululizo, hali ilikuwa mbaya sana Jumanne katika Bunge la kitaifa.

Hatama ya ofisi ya Bunge inayoongozwa na Jeanine Mabunda itajulikana Alhamisi wiki hii baada ya kambi mbili kuafikiana jana jioni kuendelea na mazungumzo.

Baada ya makabiliano makali, hali ya utulivu ilirejea Jumane jioni wiki hii. Mvutano huo umeibuka tangu Jumatatu wiki hii, siku moja baada ya rais Felix Tshisekedi kutangaza kuvunjika kwa muungano wa kisiasa kati ya miungano miwili madarakani, FCC na CACH.

Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa Desemba 6 mwaka huu, Tshisekedi alisema uhusiano huo sasa utashindwa kwa sababu ya tofauti ya kimaono katika namna ya uendeshaji wa serikali.

Rais huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri wa upinzani wa DRC, Etienne Tshisekedi, alisema mambo ambayo ushirikiano huo ulishindwa kupata uelewa wa pamoja ni masuala ya ulinzi na usalama, kinga dhidi ya wafanya maovu, rushwa na mabadiliko ya uendeshaji wa uchaguzi.

Uamuzi huo wa Tshisekedi ulitarajiwa na wengi lakini umeibua mjadala mkubwa kwa sababu ya athari za kisiasa zinazoweza kutokea na sasa kila mfuatiliaji wa siasa za DRC anatazama ni kwa vipi kiongozi huyo mchanga ataweza kuchanga karata zake.