MAREKANI-SUDAN-DIPLOMASIA

Ugaidi: Sudan yasubiri Washington kuiondoa kwenye orodha yake nyeusi

Waziri Mkuu wa Sudan  Abdalla Hamdok
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok AP / File Photo

Marekani  imetangaza kuwa itaiondoa kabisa Sudan kwenye orodha ya nchi "zinazohusika zaidi" katika suala la uhuru wa kidini. Hili ni tangazo muhimu kwa Khartoum. Lakini viongozi wa Sudan, wanasubiri Washington iondoe nchi yao kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi.

Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya mwezi mmoja baada ya kutangazwa makubaliano kati ya Sudan na Israeli, mpango wa Donald Trump unaweza  kukaribishwa.

Mamlaka ya Sudan ilisaini mkataba na Israel kwa sharti moja: hakuna uhusiano na Tel Aviv hadi Marekani itakaporejesha kinga ya kisheria ya Sudan. Kwa sasa, Khartoum bado inaweza kukabiliwa na kesi katika mahakama za Marekani kuwalipa fidia wahanga wa ugaidi.

Kwa sasa viongozi wa Sudan wanasubiri kuona hatua itakayo chukuliwa na Bunge la Marekani, ambalo katika siku zijazo linaweza kupiga kura ya sheria hii ya kinga au la.

Na kulingana na Gazeti la New York Times, utawala wa Trump na Israeli kwa sasa wanaendelea na ushawishi kwa wabunge wa Baraza la Congress. Lakini hali ni nzito kwani maseneta wawili wa chama cha Democratic wanapinga muswada huu.

Kwa sasa Washington na Tel Aviv wana wasiwasi mkubwa, ikiwa Sudan haitoondolewa kinga, huenda ikakataa kutia saini mkataba wa Abraham na Israeli, hali ambayo inaweza kuchochea uhasama na kusitisha mpango wa Israeli wa maridhiano na nchi za Kiarabu.