DRC-SIASA-SPIKA

Hatma ya ofisi ya Bunge DRC kujulikana Alhamisi

Jeanine Mabunda, spika wa bunge nchini DRC, akiapa katika majengo ya bunge mwaka 2018
Jeanine Mabunda, spika wa bunge nchini DRC, akiapa katika majengo ya bunge mwaka 2018 ©JUNIOR D. KANNAH/AFP

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi Tshilombo amekutana na wajumbe watatu walioteuliwa kuliongoza bunge la mpito nchini humo baada ya kushuhudia hali ya utulivu kwenye Bunge la nchi hiyo, ambapo mvutano huo uliibuka tangu Jumatatu wiki hii, siku moja baada ya rais Felix Tshisekedi kutangaza kuvunjika kwa muungano wa kisiasa kati ya miungano miwili madarakani, FCC na CACH.

Matangazo ya kibiashara

Haya yanajiri wakati hatma ya ofisi ya Bunge inayoongozwa na Bi Jeanine Mabunda kujulikana hivi leo Alhamisi baada ya kambi mbili kuafikiana jana jioni kuendelea na mazungumzo juu ya namna ya kuliongoza Bunge hilo la mpito kuanzia Alhamisi wiki hiihii.

Utulivu ulirejea tangu jana, alisema Mboso mbunge ambaye anaongoza kiumri na kaongeza kuwa hatua inayofuata ni uchunguzi wa tuhuma dhidi ya spika wa Bunge Jeanine Mabunda katika mkutano huu wa leo Alhamisi, Desemba 10.

Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa Desemba 6 mwaka huu, Tshisekedi alisema uhusiano huo sasa utashindwa kwa sababu ya tofauti ya kimaono katika namna ya uendeshaji wa serikali.

Rais huyo ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri wa upinzani wa DRC, Etienne Tshisekedi, alisema mambo ambayo ushirikiano huo ulishindwa kupata uelewa wa pamoja ni masuala ya ulinzi na usalama, kinga dhidi ya wafanya maovu, rushwa na mabadiliko ya uendeshaji wa uchaguzi.

Uamuzi huo wa Tshisekedi ulitarajiwa na wengi lakini umeibua mjadala mkubwa kwa sababu ya athari za kisiasa zinazoweza kutokea na sasa kila mfuatiliaji wa siasa za DRC anatazama ni kwa vipi kiongozi huyo mchanga ataweza kuchanga karata zake.