IVORY COAST-SIASA

Henri Konan Bédié avunja baraza la mpito lililoundwa na upinzani

Rais wa zamani wa Ivory Coast  Henri Konan Bédié
Rais wa zamani wa Ivory Coast Henri Konan Bédié REUTERS/Luc Gnago

 Rais wa zamani na kiongozi mkuu wa upinzani nchini Côte d'Ivoire, Henri Konan Bédié, amelivunja baraza la mpito lililotangazwa na upinzani kupinga kuchaguliwa kwa muhula mwingine rais Alassane Ouattara.

Matangazo ya kibiashara

Bédié amependekeza pia "mazungumzo ya kitaifa" ili kutatua mivutano inayotokana na uchaguzi wa rais Alassane Ouattara.

Henri Konan Bédié alituma taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, Desemba 9, ambapo anataka mazungumzo na kusitisha baraza la 'mpito' uliotangazwa na upinzani kufuatia uchaguzi wa urais wa Oktoba 31.

"Ninapendekeza kuanzia sasa na kwa haraka, kwa makubaliano na wapinzani wote, kuandaa mazungumzo ya kitaifa. Mfumo huu mpya wa mazungumzo ambao utavishirikisha vyama vyote vya hapa nchini (...) yanachukua nafasi ya CNT (Baraza la Mpito la Kitaifa) ambalo upinzani wa Côte d'Ivoire ulikuwa umependekeza hapo awali, " amesema Henri Konan Bédié.

Siku mbili baada ya uchaguzi wa urais, ambao matokeo yake yalikuwa bado hayajatangazwa, upinzani ulitangaza kuundwa kwa 'baraza la mpito la kitaifa', ambalo lingeunda "serikali ya mpito", kuchukua nafasi ya utawala wa Alassane Ouattara. Henri Konan Bédié, ambaye alikuwa amewasilishwa kama "rais" wa CNT, hakuwahi kuzungumza hadharani juu ya suala hilo.

Novemba 3, baada ya kutangazwa kwa ushindi wa Alassane Ouattara kwa muhula wa tatu na Tume ya Uchaguzi, maafisa wa polisi walizingira makazi ya viongozi wakuu wa upinzani, ikiwa ni pamoja na makaazi ya Henri Konan Bédié.

Maafisa kadhaa, ikiwa ni pamoja na Pascal Affi N'Guessan, Waziri Mkuu wa zamani, na mshirika wa karibu wa Henri Konan Bédié, Maurice Guikahué, walikamatwa siku siku chache baadaye, na mpaka sasa bado wanazuiliwa.

Uchaguzi wa urais ulifanyika katika mazingira ya mvutano, na upinzani ulitoa wito kwa raia kutotii maagizo ya serikali mpya " na kususia uchaguzi. Kwa jumla, ghasia za uchaguzi (kisiasa na kikabila) zilisababisha vifo vya watu angalau 85 na karibu 500 walijeruhiwa nchini Côte d'Ivoire kati ya mwezi Agosti na Novemba.

Hali ya utulivu ilirejea baada ya mkutano uliofanyika Novemba 11 kati ya Alassane Ouattara na Henri Konan Bédié. Hata hivyo Henri Konan Bédié alikuwa ametangaza "kusitisha mazungumzo" mnamo Novemba 20.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bédié amesema kwamba wameafikiana kulivunja baraza la mpito lililoundwa ili kutoa mwanya kufanyika mazungumzo ya kitaifa yanayowashirikisha wadau wa kitaifa na wale wa kimataifa.