IVORY COAST

Côte d'Ivoire: Alassane Ouattara kuapishwa kwa muhula wa tatu

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara.
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara. REUTERS/Luc Gnago/File Photo

Rais Alassane Ouattara amabaye hivi karibuni alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais na Tume ya Uchaguzi anatarajia leo Jumatatu kuapishwa kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula wa tatu.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe zitafanyika katika ikulu ya rais huko Abidjan ambapo wakuu kadhaa wa nchi za Afrika wanatarajia kuhudhuria.

Rais Alassane Ouattara atakula kiapo mbele ya wajumbe wa Mahakama ya Katiba na wabunge, kabla ya kulihutubia taifa na baadae jeshi litatoa heshima lake kwa rais huyo.

Viongozi wa nchi za Afrika ambao tayari wamebaini kwamba watahudhuria hafla hiyo ni pamoja na rais wa Benin Patrice Talon, rais Togo Faure Gnassingbé, rais wa Congo Denis Sassou-Nguesso rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, rais wa sasa wa ECOWAS. Ufaransa, itawakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya nje Jean-Yves Le Drian.

Alassane Ouattara anaapishwa wakati nchi hiyo inakabiliwa na mvutano wa kisiasa, licha ya hali hiyo kutulia baada ya mkutano kati ya kiongozi wa chama cha upinzani cha PDCI Henri Konan Bédiéna rais Ouattara Novemba 11.

Wiki iliyopita, kupitia sauti ya Henri Konan Bédié, upinzani, ulitoa wito kwa mara nyingine wa 'mazungumzo ya kitaifa' yatakayowashirikisha wadau wote katika siasa, ili kurekebisha Katiba na kuandaa uchaguzi mpya. Hata hivyo chama cha RHDP cha Alasane Ouattara kilitupilia mbali hoja hiyo.