SUDAN

Waziri Mkuu Abdallah Hamdok alauamu wanajeshi kuingilia uchumi wa Sudan

Waziri mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok.
Waziri mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok. Ebrahim HAMID / AFP

Waziri Mkuu wa Sudan ameshtumu vigogo katika jeshi nchini Sudan kujihusisha katika uchumi wa nchi hiyo. Hali ambayo wengi wana hofu ya kuzuka mtafaruku nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Ukosoaji huu wa Abdallah Hamdok dhidi ya maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi huenda ukazua sintofahamu nchini humo miezi michache baada ya kumalizika kwa makubaliano ya kihistoria ya jeshi kukabidhi madaraka kwa raia, makubaliano yaliyofikiwa mwezi Agosti 2019.

Abdallah Hamdok amedhamiria kukomesha kitendo cha maafisa wakuu wa jeshi na maafisa waandamizi katika idara ya ujasusi kwa kuingilia uchumi wa nchi. Wengi wamekuwa wakiweka mbele maslahi yao.

Kwa upande wa waziri mkuu wa Sudan, amesema ikiwa ni kawaida kwa wanajeshi kuwekeza katika biashara zinazohusiana na usalama, "haikubaliki" wafanye hivyo katika sekta zingine za uchumi.

Chini ya utawala wa Omar al-Bashir, majenerali na maafisa waandamizi katika idara za usalama walijihusisha katika sekta zenye faida kubwa kama biashara za dhahabu, fizi za kiarabu, biashara ya  nyama, biashara ya unga au ufuta.

Kauli hii ya Abdallah Hamdok Jumanne, Desemba 14 ilikuja siku ambayo Washington iliiondoa rasmi Sudan kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi, hali ambayo sasa inamruhusu kufikiria nchi hiyo kufanya biashara na nchi zingine duniani na kuvutia wawekezaji.

Marekani inawahimiza viongozi wapya wa Sudan kujikita kwenye njia ya utawala bora.