RWANDA-UGIRIKI

Rwanda: Familia ya Rusesabagina yawasilisha malalamiko dhidi ya shirika la ndege la Uigiriki

Paul Rusesabagina
Paul Rusesabagina AFP Photos/Simon Wohlfahrt

Paul Rusesabagina na familia yake wamewasilisha mashitaka nchini Marekani dhidi ya kampuni binafsi ya ndege ya Uigiriki ya GainJet Aviation. Wanamshutumu kuwa imehusika kwa kile wanachokiona kama utekaji nyara wa mpinzani wa Rwanda na serikali ya Paul Kagame.

Matangazo ya kibiashara

Paul Rusesabagina na familia yake wamewasilisha mashitaka nchini Marekani dhidi ya kampuni binafsi ya ndege ya Uigiriki ya GainJet Aviation. Wanamshutumu kuwa imehusika kwa kile wanachokiona kama utekaji nyara wa mpinzani wa Rwanda na serikali ya Paul Kagame.

 

Malalamiko hayo yalifikishwa Jumatatu, Desemba 14 katika mahakama huko Texas, jimbo ambalo Paul Rusesabagina ana makazi.

 

 

Mashitaka yaliyowasilishwa mahakamani yanaitia hatiani kampuni ya GainJet, lakini pia mchungaji, Constantin Niyomwungere, anayetuhumiwa kuwa afisa wa serikali ya Rwanda.

 

Inasemekana kwamba Constantin Niyomwungere alimwalika Paul Rusesabagina kuja kuzungumzia kuhusu maswala ya haki za binadamu kwenye makanisa nchini Burundi, wakati kampuni ya GainJet inadaiwa kulipwa pesa na serikali ya Rwanda ili kumleta mkosoaji huyo wa utawala wa Kagame jijini Kigali.

 

Mawakili wa familia ya Rusesabagina wanadai kuwa wana ushahidi, bila kutoa maelezo zaidi. Wanadai kuwa kampuni ya GainJet imeshindwa kutekeleza jukumu lake la kisheria kuhakikisha usalama wa abiria wake.

 

Kwa malalamiko haya, wanatarajia kutoa mwanga juu ya mazingira ambayo bado hayajafahamika ya kukamatwa kwa Paul Rusesabagina, na hasa, kuweka shinikizo kwa jamii ya kimataifa kudai kuachiliwa kwa mpinzani huyo.

 

Wakati huo huo Waziri wa Sheria nchini Rwanda amemjibu mjumbe wa bunge la Marekani ambaye alikuwa amemwandikia Rais Paul Kagame akimtaka Paul Rusesabagina aachiliwe huru.

 

Paul Rusesabagina yuko gerezani nchini Rwanda kwa madai ya ugaidi.

 

Waziri Jonhnston Businjye amesema kuwa Rwanda ni nchi huru na haichukui maagizo kutoka mahali kwingine.