JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

CAR: Upinzani wataka uchaguzi wa Desemba 27 kuahirishwa

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Toudéra.
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Toudéra. Ludovic MARIN / AFP

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, sasa unataka uchaguzi mkuu wa Desemba 27 mwaka huu uahirishwe, tangazo linaloibua wasiwasi wa kutokea machafuko nchinik humo.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani unadai mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi huru na haki hayapo, wakimtuhumu rais Faustin-Archange Touadéra, kwa kujaribu kuharibu mchakato wa uchaguzi.

Matamshi yao wanayatoa wakati huu Serikali ikimtuhumu rais wa zamani Francois Bozize kwa kupanga njama za kutaka kuipindua Serikali.

Serikali inasema wapiganaji watiifu kwa rais wa zamani Bozize, wako kwenye mji wa Bossembele na wanapanga kuvamia mji mkuu Bangui.

Sintofahamu zaidi iliibuka majuma kadhaa nyuma baada ya mahakama ya juu nchini humo, kukataa kumuidhinisha Bozize kuwa mmoja wa wagombea katika uchaguzi wa juma lijalo.

Umoja wa Mataifa ulisema mwishoni mwa juma kuwa umetuma wanajeshi wake wa kulinda amani kwenye maeneo ambayo kuna hofu ya kutokea mapigano.

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, François Bozizé.
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, François Bozizé. REUTERS/Luc Gnago

Hadi sasa kuna taarifa kuwa wapiganaji waasi wameiteka miji kadhaa jirani namji mkuu Bangui, huku wakipigana na vikosi vya Serikali na kuharibu mali za watu, umoja wa Mataifa ukisema vikosi vyake vimejipanga kuzuia mashambulizi yoyote.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ni miongoni mwa mataifa masikini barani Afrika licha ya kuwa na utajiri wa rasilimali kama Almasi na Urani.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu nusu ya raia wa taifa hilo wanaishi kwa kutegemea misaada ya kibinadamu.

Nani wahusika hasa wa mzozo huu?

Francois Bozize, muumini wa Kikristo, aliingia madarakani baada ya mapinduzi mwaka 2003 na kuchaguliwa mara mbili mfululizo katika chaguzi ambazo zinatajwa hazikuwa huru.

Aliondolewa mamlakani mwaka 2013 na waasi wa Seleka, ambao wengi wanajumuisha Waislamu wakimtuhumu kwa kukiuka mkataba wa amani.

Tangu wakati huo taifa hilo linashuhudia hali tete ya usalama ambapo makundi ya waasi wa Seleka na Anti balaka yamekuwa yakipigana kwa misingi ya kidini.

Baada ya majeshi ya Ufaransa kuingilia kati machafuko ya nchi hiyo, uchaguzi ulifanyika mwaka 2016 na rais Faustin-Archange Touadéra, alichaguliwa tena na sasa anaomba kuchaguliwa kwa mara nyingine.

Hata hivyo mapigano kati ya makundi yenye silaha yameendelea kushuhudiwa, umoja wa Mataifa ukiyatuhumu makundi ya waasi kwa kusababisha hali tete ya usalama nchini humo.

Bozize, aalirejea nchini mwake mwezi Desemba mwaka 2019, baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka sita nchini Benin, Cameroon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kurejea kwake kuliibua wasiwasi kuhusu kuharibika kwa mchakato wa amani.

Bozize bado ana ufuasi mkubwa nchini mwake hasa katika jeshi na baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Hata hivyo anakabiliwa na vikwazo vya umoja wa Mataifa kwa kile anachodaiwa kuwaunga mkono waasi wa anti Balaka mwaka 2013.