JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Jamhuri ya Afrika ya Kati yaendelea kukumbwa na sintofahmu

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadéra, akiwa na maofisa usalama alipotembelea moja ya maeneo ya nchi yake
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadéra, akiwa na maofisa usalama alipotembelea moja ya maeneo ya nchi yake Gaël Grilhot/RFI

Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, linasema limevirudisha nyuma vikosi vya waasi, vilivyokuwa vinakwenda jijini Bangui.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja, baada ya muungano wa waasi nchini humo unaoongozwa na rais wa zamani Francois Bozize, kutaka Uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 27 kuahirishwa.

Upinzani unadai mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi huru na haki hayapo, wakimtuhumu rais Faustin-Archange Touadéra, kwa kujaribu kuharibu mchakato wa uchaguzi.

Matamshi yao wanayatoa wakati huu Serikali ikimtuhumu rais wa zamani Francois Bozize kwa kupanga njama za kutaka kuipindua Serikali.

Awali Serikali ilisema wapiganaji watiifu kwa rais wa zamani Bozize, wako kwenye mji wa Bossembele na wanapanga kuvamia mji mkuu Bangui.

Rais Faustin-Archange Touadéra akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa kampeni, amewataka vijana nchini humo kukataa kutumiwa na makundi ya waasi.

Sintofahamu zaidi iliibuka majuma kadhaa nyuma baada ya mahakama ya juu nchini humo, kukataa kumuidhinisha Bozize kuwa mmoja wa wagombea katika uchaguzi wa juma lijalo.

Umoja wa Mataifa ulisema mwishoni mwa juma kuwa umetuma wanajeshi wake wa kulinda amani kwenye maeneo ambayo kuna hofu ya kutokea mapigano.

Hadi sasa kuna taarifa kuwa wapiganaji waasi wameiteka miji kadhaa jirani na mji mkuu Bangui, huku wakipigana na vikosi vya serikali na kuharibu mali za watu, umoja wa Mataifa ukisema vikosi vyake vimejipanga kuzuia mashambulizi yoyote.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ni miongoni mwa mataifa masikini barani Afrika licha ya kuwa na utajiri wa rasilimali kama Almasi na Urani.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu nusu ya raia wa taifa hilo wanaishi kwa kutegemea misaada ya kibinadamu.