MAREKANI-LIBYA

Abou Agila Mohammad Massoud Ashtakiwa kwa tukio la Lockerbie

Eneo la ajali ya ndege aina Boeing 747 ya kampuni ya Pan Am
Eneo la ajali ya ndege aina Boeing 747 ya kampuni ya Pan Am AFP/ROY LETKEY

Marekani imemfungulia mashitaka raia wa Libya, anayedaiwa kushiriki katika shambulio la Lockerbie la mwaka 1988 dhidi ya ndege ya Pan Am, lililogharimu maisha ya watu 270, ikiwa ni pamoja na Wamarekani 190.

Matangazo ya kibiashara

Abu Agila Mohammad Massoud, afisa mwandamizi wa zamani wa idara ya ujasusi nchini Libya anayezuiliwa nchini humo, amepatikana na hatia ya mashtaka mawili yanayohusiana na shambulio hilo.

Maafisa wa Merika wamesema wana matumaini Libya itamruhusu Abu Agila Mohammad Massoud kushtakiwa nchini Merika.

Kulingana na Idara ya Sheria ya Marekani, mtuhumiwa huyo alifanya kazi kwa niaba ya idara ya ujasusi ya Libya, kama mtaalam wa kiufundi katika ujenzi wa vifaa vya kulipuka, kuanzia mwaka 1973 hadi 2011.

Idara ya Sheria pia inamshuku kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika kilabu cha usiku cha La Belle mnamo mwaka 1986 huko Berlin, nchini Ujerumani, shambulio lililoua askari wawili wa Marekani.

Mnamo 1991, maafisa wengine wawili wa idara ya ujasusi wa Libya walishtakiwa kwa kuhusika na shambulio la Lockerbie: Abdel Baset Ali El-Megrahi na Lamen Khalifa Fhimah.

Megrahi, ambaye kila wakati alidai kuwa hana hatia, alifariki dunia nchini Libya mnamo mwaka 2012, miaka mitatu baada ya kuachiliwa huru na serikali ya Scotland kwa sababu za kibinadamu baada ya kugundulika na ugonjwa wa saratani.

Pan Am Boeing 747, ambayo ilikuwa ikifanya safari zake kati ya London na New York, ililipuka juu ya anga ya mji wa Scotland, Lockerbie mnamo Desemba 21, 1988, na raia wengi wa Marekani waliokuwamo wakirudi Marekani kwa sikukuu za mwisho wa mwaka.