IVORY COAST

Cote d'ivoire yaanza mazungumzo kutafuta suluhu ya kisiasa

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara John MacDougall/Pool via REUTERS/File Photo

Serikali na upinzani nchini Cote d'Ivoire wameanza mazungumzo kumaliza mvutano wa kisiasa nchini humo, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba.

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo hayo yameanza kwa kuangazia mageuzi ndani ya Tume ya Uchaguzi kuelekea Uchaguzi wa wabunge utakaofanyika mapema mwaka 2021.

Waziri wa maridhiano ya kitaifa Kouadio Konan Bertin, amesema kuanza kwa mazungumzo hayo, kunadhihirisha wazi pande zote zinahitaji amani.

Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa katika mvutano wa kisiasa tangu mwezi Agosti, wakati rais Alassane Ouattara kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu, hatua ambayo ilipingwa vikali na wanasiasa wa upinzani waliosema ni ukiukwaji wa Katiba.

Vurugu za kisiasa zilishuhudiwa kati ya wafuasi wa upinzani na maafisa wa usalama na kusababisha vifo vya watu 85 na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa.

Licha ya pingamizi hizo, rais Ouattara aliwania tena na kuibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika mwezi Oktoba na baada ya kuapishwa tarehe na kukutana na kiongozi wa upinzani Konan Bedie, rais Outtara aliomba kufanyika kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani.