MALI

Ripoti: Jeshi la Mali lashtumiwa kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu

Viongozi wakuu wa jeshi nchini Mali wakiongozwa na Assimi Goïta, mwezi Septemba 2020
Viongozi wakuu wa jeshi nchini Mali wakiongozwa na Assimi Goïta, mwezi Septemba 2020 MICHELE CATTANI / AFP

Tume ya kimataifa ya uchunguzi kwa Mali, iliyoundwa na wataalam huru wa kimataifa, inashtumu makundi ya kigaidi yenye silaha na wanamgambo wa Dan Na Amssagou kwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti iliyowasilishwa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo imevuja kwa vyombo vya habari, tume hiyo inanyooshea kidole cha lawama pande zote kwenye mzozo huo, ikiwa ni pamoja na makundi yenye silaha ambayo yalisaini mikataba ya amani, lakini pia na hasa jeshi la Mali, kwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika kipindi kinachoanzia mwezi Januari 2012 hadi Januari 2018.

Kwa kipindi cha miaka 6, kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2018, ripoti iliyotolewa na wataalam huru wa Umoja aw Mataifa inataja visa vingi vya mauaji.

Yote haya yalianza wakati makundi yenye silaha yalianzisha mapigano dhidi ya jeshi la serikali. Moja ya matukio mabaya yalitokea Januari 24, 2012, siku hiyo huko Aguelhok kaskazini mwa Mali, muungano wa makundi ya kigaidi yaliua karibu wanajeshi 100.

Katika ripoti hiyo, ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu umeripotiwa kwa msingi wa viwango vya ushahidi wa kimataifa: mauaji ya halaiki, mauaji ya mtu mmoja mmoja, mateso na ubakaji.

Vitendo ambavyo ni uhalifu wa kivita, kulingana na Tume ya uchunguzi, na ambavyo vilifanywa na pande zote husika kwenye mzozo ikiwa ni pamoja na jeshi.

Hata hivyo jeshi la Mali linasemekana kuwa na hatia ya mauaji na vitendo vya mateso katika baadhi ya operesheni ilizofanya hasa katika mji wa Diabali, ambapo watu 16 waliuawa mwezi Septemba 2012.