JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Sintofahamu yaendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati siku chache kabla ya uchaguzi

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadéra akifanya ziara nchini mwake
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadéra akifanya ziara nchini mwake Gaël Grilhot/RFI

Maswali yameibuka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya makundi ya waasi siku chache kabla ya uchaguzi wa urais Jumapili Decemba 27.

Matangazo ya kibiashara

Wengi wanajiuliza iwapo uchaguzi huo unaweza kuahirishwa au la kufuatia hali hiyoya kudorora kwa usalama katika baadhi ya maeneo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Siku ya Jumanne makundi yenye silaha yaliendesha mashambulizi ya pamoja katika maeneo mbalimbali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wakati huo huo wanasiasa na waangalizi wa mchakato wa uchaguzi wanahoji kuhusu uwezekano wa kufanya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika siku ya Jumapili.

Hivi karibuni Urusi na Rwanda zilipeleka wanajeshi wao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya shambulio la makundi ya waasi lililodaiwa na serikali kama "jaribio la mapinduzi".

Makundi matatu kati ya makundi yenye nguvu zaidi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yalishambulia, siku ya Ijumaa, barabara muhimu zinazoelekea mji mkuu, Bangui, na kutangaza muungano wao.

Serikali ya Bangui inaendelea kumshtumu rais wa zamani François Bozizé kwa "kujaribu kupindua serikali" kwa "nia dhahiri ya kuandamana na vikosi vyake katika mji wa Bangui" wakati uchaguzi wa Jumapili unaandaliwa kote nchini.

Hata hivyo rais anayemaliza muda wake, Faustin Archange Touadéra anapewa nafasi kubwa ya kushinda, baada ya François Bozizé kukataliwa kugombea kutokana na kuwa hatimizi vigezo vya kuwania katika uchaguzi huo.