ETHIOPIA

Ethiopia: Watu 42 wauawa katika operesheni ya jeshi katika eneo la Benishangul-Gumuz

Jeshi la Ethiopia
Jeshi la Ethiopia REUTERS/Tiksa Negeri/File Photo

Watu 42 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya zaidi ya watu 100 wakiwemo watoto katika eneo la Benishangul-Gumuz wameuawa katika operesheni ya jeshi la Ethiopia, kulingana na vyanzo usalama nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Washukiwa hao wanashutumiwa kuwapiga risasi na kuwachoma visu wanavijiji waliokuwa wamelala , na kuteketeza kwa moto nyumba zao siku ya Jumatano.

Duru za kuaminika zimebaini kwamba maafisa watano wa serikali ya sasa na wenzao wa zamani wamekamatwa kufuatia tatizo hilo la kiusalama.

Naibu waziri wa serikali ni miongoni mwa watu watano waliokamatwa vilisema vyombo vya habari vya serikali.

Shambulio hilo lilitokea siku moja baada ya waziri mkuu Abiy Ahmed kuzuru mji huo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alielezea mauaji hayo kama ya kusikitisha na kusema kwamba serikali yake imetuma wanajeshi katika eneo hilo ili kutafuta suluhu ya mzozo huo.

Siku ya Jumanne Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitangaza kuanzisha operesheni mpya ya kijeshi katika jimbo la Benishandul-Gumuz, Magharibi mwa Ethiopia kwa lengo la kuyatimua makundi ya kigaidi lakini operesheni hii ilizua hofu ya kutokea kwa vita kati ya Ethiopia na Sudan.

Benishandul Gumuz, jimbo lenye wakaazi zaidi ya milioni moja kutoka makabila tofauti, limeendelea kushuhudia visa vingi vya unyanyasaji na mauaji katika miezi ya hivi karibuni.

Jamii ya walio wachache ya Amhara wanaoishi katika mkoa huo ni miongoni mwa makabila yanayolengwa na mauaji hayo.

Ethiopia imeshuhudia ongezeko la ghasia za kisiasa, kikabila na kidini katika miaka ya hivi karibuni.