DRC

Marekani yaonya juu ya kutokea kwa shambulio kubwa Beni, Mashariki mwa DRC

Jiji kuu la DRC, Kinshasa
Jiji kuu la DRC, Kinshasa REUTERS/Kenny Katombe

Washington imewaonya raia wake kuacha kusafiri kuelekea mashariki mwa DRC ambako shambulio la kigaidi limepangwa kutokea siku ya Krismasi.

Matangazo ya kibiashara

"Ubalozi wa Marekani jijini Kinshasa umepokea habari ya kuaminika juu ya uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi siku ya Krismasi (Desemba 25, 2020) dhidi ya makanisa na maeneo mengine ambayo watu wasio Waislamu hukusanyika katika jiji la Beni, katika mkoa wa Kivu Kaskazini, DRC, "imesema taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti ya uwakilishi wa kidiplomasia wa Marekani.

"Tunaendelea kuonya raia wa Marekani wasisafiri kwenda katika mkoa wa Kivu Kaskazini," imebaini hati hiyo.

Kundi la Islamic State hapo awali lilidai kuhusika na mashambulizi yaliyofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la waasi wa Uganda la ADF (Allied Democratic Forces) ambalo hivi karibuni lilitangaza kuungana na kundi la Islamic State.

Mnamo mwezi Oktoba, watu wenye silaha kutoka kundi hili walishambulia gereza la Kangabay huko Beni na kusababisha wafungwa zaidi ya 1,300 kutoroka. ADF pia iliendesha shambulio lingine wakati huo huo dhidi ya ngome za jeshi la DRC, FARDC.