JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-UCHAGUZI

Jamhuri ya Afrika ya Kati kufanya uchaguzi licha ya kudorora kwa usalama

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati  Faustin-Archange Touadéra, anayewania tena urais
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra, anayewania tena urais RFI/Romain Ferré

Uchaguzi Mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati unafanyika Jumapili hii, Desemba 27, wakati hali ya usalama bado ni tete.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano yaliripotiwa jana, Ijumaa, katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na huko Dékoa. Umoja wa Mataifa unasema umepoteza askari wake watatu kutoka Burundi, waliouawa na "wapiganaji wenye silaha wasio julikana".

Wagombea kadhaa kwenye uchaguzi wa Jumapili wamesema wanajiengua kutokana na sababu za kiusalama.

Wengi wa wakaazi wa mji mkuu, Bangui, wanasema hali ya usalama haitoshelezi kuhakikisha uchaguzi salama siku ya Jumapili.

Muungano wa makundi yenye silaha wa CPC unaonekana kuazimia kuvuruga uchaguzi. Pamoja na hayo, mamlaka na taasisi za kimataifa wanasisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa Jumapili Decemba 27.

Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi na Ukarabati wa Nchi, Marie-Noëlle Koyara amejaribu kutuliza wasiwasi wa umma.

"Tunasikitika kulazimika kuja kuilaani hali hii. Uchaguzi ni haki ya kikatiba. Serikali inajipanga, tutatumia vikosi vyetu vyote ili usalama na utulivu urudi nchini mwetu."

Muungano wa CPC uliundwa Disemba 19 na makundi yenye silaha yaliyomtuhumu Rais Faustin Archange Touadera kuwa na njama ya udanganyifu kwenye uchaguzi huo wa Jumapili ambako rais na Wabunge watachaguliwa.