JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Jamhuri ya Afrika ya Kati yafanya uchaguzi licha ya wasiwasi wa usalama

Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wapiga kura
Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wapiga kura Centre for Humanitarian Dialogue

Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanamchagua rais wao mpya pamoja na wabunge leo Jumapili Desemba 27, licha ya hali ya usalama kuwa hatarini kutokana na mapigano ya hivi karibuni kati ya vikosi vya serikali na muungano wa makundi ya waasi ambayo yalitaka uchaguzi huo uahirishwe.

Matangazo ya kibiashara

Wanamgambo wanaompinga Rais Faustin-Archange Touadera, ambaye anatafuta muhula wa pili madarakani, wamezidisha mashambulizi tangu mahakama ya katiba ilipotupilia mbali baadhi ya wagombea, akiwemo rais wa zamani, Francois Bozize, mapema mwezi huu.

 

Mgogoro huo umesababisha wakaazi wengi katika taifa hilo lenye utajiri wa almasi na dhahabu kushikwa na hofu ya kutumbukia tena katika machafuko kama yaliyotokea miaka ya nyuma.

 

Uchaguzi wa Jamhuri ya Afrika ya kati umetajwa kuwa mtihani muhimu kwa nchi hiyo yenye matatizo makubwa ya usalama.

Muungano wa CPC uliundwa mwezi Desemba tarehe 19 na makundi yenye silaha, yanayomshutumu rais Faustin Archange Touadera, kwa kujaribu kufanya udanganyifu katika uchaguzi mkuu unaofanyika leo Jumapili Desemba 27 ili asalie madarakani.

Rais Faustin, anatarajiwa kushinda uchaguzi huo.

Makundi ya wapiganaji yanadhibithi Theluthi tatu ya Jamhuri ya Afrika ya kati, ambayo sehemu kubwa ya watu ni maskini sana.

Serikali imemshutumu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Francois Bozize kwa kupanga kupindua utawala wa Faustin Archange Touadera. Bozize ameendelea kukana madai hayo.

Wagombea wawili wa urais, Eloi Anguimaté na Aristide Briand Reboas, wamezungumza na vyombo vya habari, na kuelezea wasiwasi wao juu ya maandalizi ya uchaguzi huo wa Disemba 27. Hali kadhalika wagombea wote wa ubunge kutoka Lobaye kusini mwa nchi walijiunga na miito ya kutaka uchaguzi huo uahirishwe.

Rais wa sasa Faustin Archange Touadera anatarajia kushinda na kuchukuwa muhula wa pili madarakani, akiwapiku wapinzani 15 waliojitosa katika kinyang'anyiro hicho cha urais.

Kulingana na maoni ya wakaazi wa mji mkuu, Bangui, hali ya usalama haitoshelezi kuhakikisha uchaguzi salama siku ya Jumapili. Huko Bambari, eneo la katikati mwa nchi ambalo ni kitovu cha mapigano, wapo wanajeshi wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, MINUSCA, lakini pia na wanamgambo waasi ambao wamejihami.

Jana Jumamosi Mahakama ya Katiba ilikataa kuahirishwa kwa uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mahakama ya Katiba inasema kuwa kuahirisha kwa Uchaguzi Mkuu hakutaheshimu muda uliowekwa na

katiba kwamba rais mpya anapaswa kuwa amekabidhiwa madaraka ifikapo Machi 30.