JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Jamhuri ya Afrika ya Kati: Uchaguzi wafanyika licha ya vitisho vya waasi

Mpîga  kura nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Disemba 27 2020
Mpîga kura nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Disemba 27 2020 Centre for Humanitarian Dialogue

Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaendelea kusubiri uamuzi wa Tume ya uchaguzi kuhusu uchaguzi uliofanyika Jumapili Desemba 27, baada ya kuonekana kuwa kuna baadhi ya vituo vya kupigia kura havikufunguliwa, huku baadhi ya wapiga kura wakisalia nyumbani kwa hofu ya kuuawa katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na vyanzo rasmi kutoka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, vituo 800 vya kupigia kura havikufunguliwa nchini kote kwa jumla ya vituo 5,400, sawa na asilimia 15.

Licha ya matatizo kadhaa yaliyojitokeza, uchaguzi ulifanyika kwa amani katika mji mkuu wa Jamhuri ay Afrika ya Kati, Bangui, na katika baadhi ya miji mikubwa.

Milio ya risasi ilisikika katika mji wa Bangui usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, lakini hali ya usalama ilirudi kuwa shwari, baada ya vikosi vya usalama kupelekwa katika maeneo mbalimali ya mji huo vikisaidiwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa Rwanda.

Hivi karibuni wanamgambo wanaompinga rais Faustin-Archange Touadera, ambaye anatafuta muhula wa pili madarakani, walizidisha mashambulizi tangu mahakama ya katiba ilipotupilia mbali baadhi ya wagombea, akiwemo rais wa zamani, Francois Bozize, mapema mwezi huu.

Mgogoro huo ulisababisha wakaazi wengi katika taifa hilo lenye utajiri wa almasi na dhahabu kushikwa na hofu ya kutumbukia tena katika machafuko kama yaliyotokea miaka ya nyuma.

Uchaguzi wa Jamhuri ya Afrika ya kati ulitajwa kuwa mtihani muhimu kwa nchi hiyo yenye matatizo makubwa ya usalama.

Makundi ya wapiganaji yanadhibithi Theluthi tatu ya Jamhuri ya Afrika ya kati, ambayo sehemu kubwa ya watu ni maskini sana.

Serikali imekuwa ikimshutumu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Francois Bozize kwa kupanga kupindua utawala wa Faustin Archange Touadera. Bozize alikana madai hayo.

Rais mpya atakabidhiwa madaraka ifikapo Machi 30, 2021.