NIGER

Zoezi la uhesabuji kura laanza Niger

Wapiga kura nchini Niger
Wapiga kura nchini Niger YouTube/AFP

Siku moja baada ya wananchi wa Niger kushiriki Uchaguzi Mkuu kumchagua rais mpya na wabunge 171 watakaohudumu katika awamu mpya ya uongozi, zoezi la kuhesabu kura limeanza.

Matangazo ya kibiashara

Zoezi hilo lilianza tangu jana usiku baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa.

Kwa mara ya kwanza uchaguzi huu ulihusisha wagombea wengi zaidi wa kuwania kwenye kiti cha urais. Jumla ya wagombea 30 walishiriki kinyang'anyiro hiki cha urais.

Uchaguzi wa rais na bunge, kwa mara ya kwanza, utawezesha kukabidhiana madaraka kwa amani tangu kupata uhuru miaka 60 iliyopita kutoka Ufaransa.

Rais wa zamani Mahamane Ousmane, Salou Djibo, ambaye aliwahi kuwa rais wa kipindi cha mpito baada ya mapinduzi, mawaziri wakuu wa zamani Amadou Boubacar Cisse na Seini Oumarou, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani Bazoum Mohamed, na Waziri wa zamani wa Mambo ya nje Ibrahim Yacoubou ni miongoni mwa wagombea katika uchaguzi huo wa urais.

Hata hivyo wagombea kiti cha urais wako 17 ambao wameshindana kuchukua nafasi ya Mahamadou Issoufou anaekamilisha muhula wake wa pili

Rais wa sasa, Mahamadou Issoufou, hakuwania kwenye nafasi hiyo kwa sababu tayari amekamilisha muhula wake wa 2 madarakani.

Hama Amadou wa chama cha upinzani cha Lumana aliyekuwa Spika wa zamani na Waziri Mkuu mara mbili aliye kuwa akichukuliwa kuwa mshindani mkubwa kwenye uchaguzi wa urais aliondolewa kwa madai kwamba alihukumiwa kifungo cha miezi 12 kutokana na kashfa ya biashara haramu ya Watoto hapo mwaka 2017.

Kutakuwa na duru ya pili pindi hakuna mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 za kura.

Niger ni mojawapo ya mataifa maskini duniani licha ya utajiri mkubwa wa madini, inakabilwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na hasa mashambulio ya wanamgambo wenye itikadi kali za kislamu kutoka nchi jirani za Mali na Nigeria.