WHO-ETHIOPIA

ETHIOPIA: Mkurugenzi wa WHO akiri kuguswa na machafuko ya nchini mwake

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus REUTERS/Denis Balibouse

Katika matamshi yake ya kwanza binafsi, mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameeleza maumivu aliyonayo kuhusu mzozo unaoendelea nchini mwake Ethiopia, kuhusu eneo la Tigray.

Matangazo ya kibiashara

"Ukiachilia ugonjwa wa Covid 19, mwaka 2020 umekuwa mgumu sana kwangu sababu nchi yangu ina matatizo," alisema Tedros wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu ya wiki hii.

Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiyi Ahmed, ambaye mwaka jana alishinda tuzo ya amani ya Nobel, aliagiza wanajeshi kuvamia mji wa kaskazini mwa nchi hiyo Tigray Novemba 4, akidai operesheni iliyofanyika ni kujibu mashambulizi ya kambi ya wanajeshi wa Serikali, yaliyofanywa na wapiganaji wa chama cha TPLF, kinachoongoza eneo hilo.

Mapigano kwenye mji wa Tigray, yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha hii ni kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya mizozo, huku maelfu wengine wakikimbilia nchi jirani kuwa wakimbizi.

Tedros ambaye mwenyewe asili yake ni watu wa Tigray, amesema ana ndugu wengi sana kwenye eneo hilo, akiwemo kaka yake ambaye anasema hadi sasa hafahamu mahali aliko.

"Sijawasiliana nao kwasababu kule kwa sasa hakuna mawasiliano."

Serikali ya Ethiopia, ilidhibiti mawasiliano kwenye eneo la Tigray, ambalo limekuwa bila mawasiliano kwa zaidi ya wiki 6 sasa huku mapigano kati ya vikosi vya Serikali na wapiganaji wa TPLF yakiripotiwa.

Mwezi uliopita, serikali ya Ethiopia, ilimtuhumu Tedros ambaye mwaka 2005 hadi 2012 alihudumu kama waziri wa afya nchini humo wakati wa utawala wa kiongozi wa TPLF marehemu waziri mkuu Meles Zenawi, kwa kushirikiana na viongozi wa eneo hilo kuwapatia silaha.

Tedros amekanusha madai dhidi yake kupitia ukurasa wa kijamii wa Twitter, akisema yeye akiwa mtoto alishuhudia maafa ya vita na amekuwa akihubiri amani tangu wakati huo.