ETHIOPIA

Ethiopia: Mapigano yaendelea katika maeneo ya vijiji vya jimbo la Tigray

Vikosi maalum vya jeshi la Amhara vinavyopambana na vile vya jimbo la  Tigray People's Liberation Front (TPLF).
Vikosi maalum vya jeshi la Amhara vinavyopambana na vile vya jimbo la Tigray People's Liberation Front (TPLF). Tiksa Negeri/Reuters

Mapigano yanaendelea katika mkoa wa Tigray, karibu miezi miwili baada ya kuzuka kwa mapigano katika jimbo hilo linalotaka kujitenga.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Ethiopia inahakikisha kuwa hali ni shwari katika mkoa huo, lakini ni vigumu kuingia katika jimbo hilo Tigray.

Hata hivyo misafara ya magari ya mashirika ya misaada ya kibinadamu imeendelea kuingiza misaada ya chakula lakini hali bado ni tete na mawasiliano mpaka sasa yamekatwa.

Vikosi vya TPLF pia vinaendelea na vita, kutoka maeneo ya vijijini.

Wakati jeshi la Ethiopia linadhibiti miji kuu ya jimbo la Tigray, hofu  inaendelea katika vijijini vya jimbo hilo.

Katika eneo la bara, bado ni ngumu kubaini ni maeneo yapi chini ya udhibiti wa serikali na ambayo yako mikononi mwa TPLF, chama kilichopinga Tigrayan kinachopigana na Addis Ababa.

Vyanzo kutoka mashirika ya kutoa misaada vinaripoti kuewepo na mapigano katika maeneo ya vijijini, hasa karibu na mji wa Shire.

Umoja wa Mataifa unasema mapigano yanaripotiwa Mashariki mwa mji wa Mekele, mji mkuu wa jimbo la Tigray.

Taarifa hiyo imethibitishwa na wakaazi wa baadhi ya maeneo ya mji huo, ambao pia wamekiri kwamba eneo la kaskazini mwa jiji bado liko kwenye vita.

Afisa mmoja wa serikali ya Ethiopia amekiri kwamba wanamgambo wa Tigray bado wanakabiliana na vikosi vya serikali.

Serikali ya shirikisho imeanzisha utawala wa muda huko Tigray, ambayo inadai kuwa huduma za msingi zimeanza tena kutolewa.