AFRIKA-COVID 19

Namna janga la Covid 19 lilivyoathiri uchumi wa mataifa ya Afrika

Kirusi cha Corona
Kirusi cha Corona NEXU Science Communication | Reuters

Licha ya bara la Afrika, kutoshuhudua maambukizi makubwa na maafa yanayotokana na janga la Covid 19, mataifa mengi katika bara hilo, yameendelea kushuhudia kuyumba kwa uchumi kutokana na kuendelea kuongezeka kwa virusi hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kuzuka kwa maambukizi hayo mapema mwaka huu, Shirika la fedha duniani IMF lilitangaza kuwa uchumi wa bara la Afrika, ungeshuka kwa asilimia tatu, lakini utakua kwa asilimlia 3.1 mwaka 2021.

IMF inasema uchumi katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania umeyumba lakini zimekuwa zikionesha dalili za kuimarika.

Mataifa yenye utajiri wa mafuta kama Algeria, Angola na Nigeria, yameathirika pakubwa kufuatia kushuka kwa bei ya mafuta ghafi duniani.

Afrika Kusini, taifa la pili kwa ukubwa wa uchumi barani Afrika, ndilo lililoathirika zaidi kwa sababu lilianza kupitia hali ngumu ya kiuchumi hata kabla ya kuzuka kwa maambukizi ya Corona na wiki hii, nchi hiyo imeripoti visa zaidi ya Milioni moja na kuwa nchi yenye maambukizi makubwa barani Afrika.

Hata hivyo, hali ni mbaya kwa mataifa yenye madeni makubwa kama Zambia, nchi ambayo inategemea sekta ya madini ili kuimarisha uchumi wake huku mataifa mengine kama Ushelisheli, Tunisia na Morocco yakipitia wakati mgumu kwa kukosa watalii.