ULAYA-AMERIKA-AFRIKA

Dunia yakaribisha mwaka mpya 2021, huku mamilioni ya watu wakiwa ndani

Raia ulimwenguni kote wanalazimika kusherekea mwaka mpya wakiwa majumbani tofauti na miaka ya nyuma, wakati huu mataifa yakitangaza makataa zaidi ya kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya Covid 19.

Mataifa mengi duniani yamesherekea mwaka mpya watu wakiwa nyumbani
Mataifa mengi duniani yamesherekea mwaka mpya watu wakiwa nyumbani France24Screenshot
Matangazo ya kibiashara

Ufyatuaji wa fataki na mikusanyiko mikubwa imepigwa marufuku kwenye nchi nyingi, kuanzia Sydney, Australia hadi New York nchini Marekani.

Sherehe nyingi zimefutwa barani Ulaya, wananchi wakiukaribisha mwaka kimya kimya, wakati huu kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa maambukizi zaidi.

Nchi ya Ufaransa yenyewe imehamasisha askari zaidi ya laki 1 ambao watakuwa na jukumu la kuzuia sherehe za aina yoyote ile hasa wakati wa muda wa kutotembea usiku.

Zaidi ya watu milioni 1 na laki 8 duniani wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huu tangu ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka mmoja uliopita nchini China.

Zaidi ya watu milioni 81 wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivi duniani kote.

Mataifa ya awali kabisa kuukaribisha mwaka mpya ni nchi ya Australia, lakini safari hii miji yote imekuwa kimya, lakini fataki zilifyatuliwa huku wananchi wakizuiwa kukusanyika.

Wananchi wengi kwenye mataifa ambayo yametangulia kuukaribisha mwaka, walishuhudia matukio ya ufyatuaji fataki kupitia televisheni.

Barani Afrika mataifa kadhaa pia yametangaza kuzuia sherehe za kukaribisha mwaka mpya kwa hofu ya mambukizi.