DRC-UN-RWANDA

UN yathibitisha kufanyika kwa operesheni za jeshi la Rwanda DRC mwaka 2020

Jeshi la Umoja wa Mataifa MONUSCO, Mashariki mwa DRC
Jeshi la Umoja wa Mataifa MONUSCO, Mashariki mwa DRC © Samir Tounsi / AFP

Jeshi la Rwanda lilifanikiwa kutekeleza operesheni kadhaa Mashariki mwa DRC mwaka 2020, kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa, wanaohusika na kuhakikisha vikwazo vya silaha  vinaheshimishwa, limebaini katika ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na Baraza la Usalama tarehe 23 Desemba.

Matangazo ya kibiashara

Operesheni hizi zinazokiuka vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya DRC, kwani Kinshasa wala Kigali hawajatoa taarifa yoyote kwa Umoja wa Mataifa.

Miongoni mwa ushahidi uliyotolewa kuhusiana na kuwa jeshi la Rwanda lilifanya operesheni kadhaa za kijeshi nchini DRC mnamo mwaka 2020, ni picha, ambayo kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa linasema linayo.

Katika picha hii, anaonekana askari wa DRC, aliyetambuliwa kama Kanali Claude Rusimbi, na wanajeshi 13 wa Rwanda.

Picha hiyo ilipigwa mnamo mwezi Mei, wakati Kanali Rusimbi alikuwa akihudumu, kulingana na wataalam, kama afisa wa uhusiano kati ya FARDC (vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na kikosi cha Rwanda kilichokuwa kikiendesha operesheni zake katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Ushahidi mwingine ambao unakuja kuthibitisha kuhusika kwa Rwanda katika operesheni dhidi ya waasi wa Kihutu wa Rwanda, ni nyaraka, picha zilizopigwa kutoka angani, na mahojiano ishirini na wanajeshi wa DRC kutoka kikosi cha MONUSCO, watafiti na wajumbe  wa mashirika ya kiraia.

Uwepo huu hata hivyo ulionyeshewa kidole na mkuu wa jeshi la FARDC mnamo mwezi Aprili 2020. Katika barua iliyowasilishwa kwa Jumuiya ya kimataifa juu ya eneo la Maziwa Makuu, inataja ukiukaji wa mpaka na uwepo wa kambi ya jeshi la Rwanda huko Kabara, katika eneo la Nyiragongo.

Hivi majuzi, mnamo Oktoba 2, 2020 kulingana na ripoti hiyo, wapiganaji 60 wa RDF (Kikosi cha Ulinzi cha Rwanda) wakiwa na bunduki 18 za kivita na roketi nne walionekana kwenye Mlima Rugomba, katika eneo la Rutshuru.

Serikali ya DRC haikabiliwi na vikwazo, lakini msaada wowote katika silaha au wanajeshi wa kigeni lazima ujulishwe rasmi kwa kamati ya inayohusika na vikwazo.

Ikihojiwa na wataalam, serikali ya Rwanda ilikana kwa maandishi kuhusiana na uwepo wa wanajeshi kwenye ardhi ya DRC. Mamlaka ya DR Congo, hata hivyo, hawakujibu jopo la wataalamu wakati ripoti hiyo ilitolewa.