DRC

DRC: Kiongozi wa zamani wa kivita Roger Lumbala akamatwa na kushtakiwa Paris

Mwanasiasa wa upinzani wa DRC  Roger Lumbala.
Mwanasiasa wa upinzani wa DRC Roger Lumbala. Screensot/youtube

Mahakama moja ya kupambana na ugaidi nchini Ufaransa imethibitisha kukamatwa kwa mbabe wa zamani wa kivita wa DRC Roger Lumbala, jijini Paris mwishoni mwa juma lililopita, huku akishitakiwa kwa uhalifu wa kivita katika ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka 2003, iliyoitwa Mapping.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mahakama hiyo inayojihusisha na mapambano dhidi ya ugaidi iliyoko jijini Paris nchini Ufaransa imefahamisha kuwa kiongozi huyo wa kundi la zamani la waasi na mkuu wa chama cha RCD-Nationale.

Roger Lumbala alikamatwa wiki iliyopita huko Paris katika hoteli moja ya kifahari na kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita ulioandikwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa ijulikanayo kwa jina la Mapping, ambapo inadaiwa uhalifu huo ulifanywa kati ya mwaka 1993 na 2003.

Kwa mujibu wa tangazo la mahakama hiyo, Lumbala ameshitakiwa kuongoza operesheni iliyofahamika kama “Effacer le Tableau” (Futa Ubao), operesheni ambayo ililenga idadi kubwa ya raia huko Ituri kati ya mwezi Julai 2002 na Januari 2003, mashtaka ambayo yanachunguzwa na majaji wa mahakama jijini Paris.

Ripoti hii inabainisha kuwa kati ya tarehe 12 na tarehe 29 Oktoba 2002, wapiganaji wenye silaha walioongozwa na Roger Lumbala wakishirikiana na wapiganaji wake Jean-Pierre Bemba kiongozi wa chama cha MLC waliwauwa raia wasiopungua 173 wa kabila la Wanande pamoja na Mbilikimo kwenye mji wa Mambasa na katika vijiji vinavyopakana na wilaya ya Beni.

Wapiganaji hawa wanasemekana walijihusisha na vitendo vya ulaji wa nyama za binadamu, uporaji mkubwa na Ubakaji.

Kwa upande wake Lumbala ameiambia mahakama hiyo makosa hayo yote yalifutwa kufwatia sheria ya msamaha iliyotangazwa na serikali mwaka 2014 ili kuruhusu upatikanaji wa amani na maridhiano ya kitaifa.