DRC-USALAMA

Waasi wa ADF wawauwa watu 21 Mashariki mwa DRC

Kijiji cha  Halungupa kilichowahi kushambuliwa na waasi wa ADF  Wilayani Beni mwaka 2020
Kijiji cha Halungupa kilichowahi kushambuliwa na waasi wa ADF Wilayani Beni mwaka 2020 RFI/Patient Ligodi

Watu 21 wameuawa, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kushambuliwa na waasi wa ADF, kundi ambalo limelaumiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu mwaka 2020.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti kutoka jeshi la Umoja wa Mataifa MONUSCO, imesema kuwa watu hao wameuawa katika kijiji cha Mwenda, eneo la Rwenzori.

Hata hivyo, kiongozi wa eneo hilo Donat Kibwana, amesema ni watu 22 ndio waliopoteza maisha, 10 wakiwa ni wanawake.

Aidha, Kibwana amesema kuwa watu 10 wamejeruhiwa  katika shambulizi hili la hivi punde dhidi ya raia Wilayani Beni.

“Watu 10 wamejeruhiwa na wengine hawajulikani waliko,” amesema Kibwana.

Haya ni mauaji ya pili ndani ya wiki moja, tangu mwaka mpya wa 2021 ulipoanza, baada ya yale yaliyotokea katika kijiji cha Tingwe.

Kundi la waasi wa ADF limelaumiwa kusababisha vifo vya watu karibu 800 mwaka 2020 katika jimbo la Kivu Kaskazini na Ituri, maeneo ambayo yanapakana na Uganda.