DRC-COVID 19

Changamoto ya umeme yatatiza vita dhidi ya Covid 19 nchini DRC

Watu wachukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya corona nchini DRC
Watu wachukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya corona nchini DRC © Siegfried Forster / RFI

Kamati ya pamoja inayosimamia vita dhidi ya maambukizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inasema kuwa vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo, vinakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya kamati hii, inakuja wakati huu nchi hiyo ya Afrika ya Kati, inapoendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi na vifo, vinavyotokana na janga la Covid 19.

Changamoto hii ya umeme pamoja na uhaba wa gesi aina ya Oxygen, zinaelezwa na kamati hii inayoongozwa na Profesa Jean-Jacques Muyembe, kuwa ni miongoni mwa sababu zinazorudsha nyuma vita dhidi ya janga hilo.

Aidha, Muyembe ameongeza kuwa, kutokana na changamoto ya umeme, inakuwa vigumu kwa kiwanda kilichopo jijini Kinshasa, kutenegeza oxygen ya kutosha.

Nchi hiyo ina maambukizi, zaidi ya Elfu 18 na vifo karibu Mia sita, huku jiji kuu Kinshasa likiendelea kuathiriwa zaidi.

Tangu, Desemba 18 mwaka uliopita, serikali ilitanagza hali ya kutotoka nje kote nchini humo kati ya saa tatu usiku na saa kumi na moja Alfajiri.

Shule  zimefungwa na haijulikani ni lini masomo yatarejelewa tena.