GHANA

Nana Akufo-Addo aapa kuongoza kwa muhula wa pili, wabunge wazozana

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo.
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo. John MacDougall/Pool/AFP via Getty Images

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, ameapishwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Desemba mwaka uliopita dhidi ya rais wa zamani John Mahama, ambaye alidai kuibiwa kura.

Matangazo ya kibiashara

Rais Nana Akufo-Addo, amewashukuru raia wa nchi yake kwa kumchagua tena.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu na watu wa Ghana kwa kunirejesha tena madarakani kwa muda wa miaka minne, hii ni ishara  kubwa ya imani  yenu kwangu, na mmeonesha kuwa mmetambua kazi kubwa na mafanikio tuliyopata muhula uliopita lakini pia mnaamini katika, kazi kubwa inayotusubiri katika kipindi cha miaka minne ijayo,” alisema.

Hafla ya kumwapisha rais Akufo Addo zimefanyika katika majengo ya bunge ambayo yalishuhudia vurugu.

Siku ya Jumatano usiku, jeshi limelazimika kuingilia kati mzozo kati ya wabunge ili kurejesha hali ya utulivu kati ya wale wa chama kilicho madarakani cha NPP na kile cha upinzani cha NDC.

Mvutano uliongezeka wakati wa kuchaguliwa kwa spika wa bunge.

Waangalizi tayari wamefananisha tukio hilo na lile lililotokea nchini Marekani baada ya wafuasi wa Donald Trump kuvamia majengo ya Bunge la Congress na kuwataka maseneta waondoke, wakati walikuwa katika kikao cha kuidhinidha ushindi wa Joe Biden kama rais wa Marekani.

Waghana wameshuhudia matukio ya machafuko katika Bunge usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii. Waliona wabunge wao wakipigana wao kwa wao walipokusanyika kumchagua spika mpya wa Bunge.

Utaratibu wa kumchagua spika mpya wa bunge ndio chanzo cha uhasama huo. Chama cha wengi, NPP, kilikuwa kimetaka kura iwe ya wazi, wakati chama cha upinzani, NDC, kilikuwa kimesisitiza kura iwe ya siri.

Katika mvutano huo, mbunge kutoka chama tawala alijaribu kuvamia sanduku la kura lililokuwa na kura wakati wa uchaguzi wa spika wa Bunge. Na mwishowe mbunge kutoka chama cha upinzani cha NDC ndiye alichaguliwa kuwa spika mpya wa Bunge hilo.

Baadhi tayari wamesema ni aibu kwa demokrasia nchini Ghana, kwa sababu jeshi halingelazimika kuingilia kati katika ukumbi wa Bunge ili kurejesha hali ya utulivu.

"Jeshi halina nafasi hapa," wamekuwa awkiimba wabunge wa upinzani ambao wanaona hatua hiyo ya jeshi kama jaribio la serikali kutaka kusalia madarakani.