DRC

Waliohukumiwa kifo kwa kumuua rais wa zamani wa DRC waachiliwa huru

Kanali Eddy Kapend baada ya kuachiliwa huru
Kanali Eddy Kapend baada ya kuachiliwa huru Arsene Mpiana / AFP

Watu 22  wakiongozwa na Kanali Eddy Kapend, aliyekuwa msaidizi wa rais wa zamani wa DRC Laurent-Désiré Kabila, waliokuwa wamehukumiwa kifo baada ya kukutwa na hatia kumuua rais huyo mwaka 2001, wameachiliwa huru baada ya kupata msamaha wa rais Felix Tshisekedi.

Matangazo ya kibiashara

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalishtumu namna Mahakama ya kijeshi ilivyoendesha kesi dhidi ya watu hao na kutoa hukumu hiyo.

Kumekuwa na shamrashamra jijini Kinshasa baada ya kuachiliwa huru kwa watu hao 22 katika gereza la Makala , na kupokelewa na mamia ya jamaa, ndugu na marafiki.

Raia wengi nchini DRC wamekuwa wakiamini kuwa watu hao waliopewa adhabu hiyo, hawakuhusika na kifo cha rais huyo wa zamani na walikuhumiwa kimakosa.

Rais wa zamani, Joseph Kabila, ambaye alichukua madaraka baada ya kuuawa kwa baba yake, mara kadhaa alikataa wito wa kuachiliwa huru kwa wafungwa hao, licha ya wengine 11 kupoteza maisha wakiwa gerezani.

Naibu Waziri wa sheria Bernard Takaishe aliyewapokea wanaume hao, nje ya Gereza hilo, amesema, waliachiliwa kwa sababu za kibinadamu.