DRC

Waliohukumiwa kwa mauaji ya Kabila wataka kesi mpya

Gereza la Makala nchini DRC
Gereza la Makala nchini DRC FP PHOTO / JUNIOR D. KANNAH

 Nchini DRC, watu 23 waliopatikana na hatia ya kesi ya mauaji ya Laurent-Désiré Kabila Januari 2001 wako huru tangu Ijumaa (Januari 8), baada ya rais Félix Tshisekedi kuamua kutoa msamaha kwa wafungwa wakisiasa mwishoni mwa mwezi Desemba 2020.

Matangazo ya kibiashara

Maafisa wao wa zamani katika utawala wa rais Laurent-Désiré Kabila, licha ya kuachiliwa huru, wanataka kesi mpya kuhusiana na mauaji ya rais huyo.

Kama walivyokuwa wakisema wanaharakati wengi, baadhi ya wafungwa hawa bado wanadai kuwa hawana hatia.

Mashaka bado yapo kuhusu hatia ya wafungwa wa zamani. Majaji wa Mahakama ya Kijeshi wakati huo iliamua kwamba licha ya hukumu kwa wafungwa hao, uchunguzi haukuwa umefungwa na jukumu la kila mmoja katika mauaji hayo halikuwekwa wazi.

Pascal Maregani mmoja wa maafisa wa usalama wa Laurent-Désiré Kabila ambaye aliachiliwa huru kwa msamaha wa rais Tshisekedi, ambaye ni miongoni mwa wafungwa hao, amebaini kwamba wakati wa mauaji hayo hakuwa nchini.

Amedai kuwa hana hatia. Baada ya kuzuiliwa miaka ishirini, sasa anataka kesi hiyo ifunguliwe tena.

“Tungependa kujua ukweli. Kwa sababu sisi ndio tulishushiwa mzigo wa lawama katika mauaji ya rais Laurent-Désiré Kabila.

Mimi kwa upande wangu, ningependa kujua ni nani aliyehusika na kitendo hiki cha kinyama. Tulimuweka mamlakani, tulifanya naye kazi, tukamlinda, hatuwezi kukubali auawe. Ikiwa kesi mpya itafunguliwa, tutafurahi na turidhika kujua ukweli, " Pascal Maregani mmoja wa maafisa wa usalama wa Laurent-Désiré amesema.

Marcelin Chikuru ambaye alifanya kazi katika Ofisi ya rais wa Jamhuri kama mkaguzi wa Idara ya Ujasusi, anasema pia anataka ukweli ujulikane.