JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Bouar yakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu licha ya hali ya utulivu kurejea

Wanajeshi wa MINUSCA wanaolinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wanajeshi wa MINUSCA wanaolinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MARCO LONGARI / AFP

Wiki iliyopita, makundi yenye silaha (anti-balaka na kundi la waasi la 3R ) yalianzisha mashambulio katika mji wa Bouar, kilomita 450 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Jamhuri ya afrika ya Kati, Bangui.

Matangazo ya kibiashara

Jumamosi waasi wa makundi hayo yalijaribu kuvamia kambi ya jeshi la Jamhuri ya afrika ya Kati pamoja na kambi ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo, Minusca, lakini wakarudishwa nyuma.

Shambulio hilo lilisababisha baadhi ya raia kuyatoroka makaazi yao na wengine kulazimika kusalia majumbani kwao, huku wengine wakikimbilia katika makanisa  ya mji wa Bouar.

Kulingana na vyanzo vya usalama siku ya Jumapili hali ya utulivu ilirejea katikamji wa Bouar. Mitaa imebaki tupu, watu wana hofu ya kutokea mapigano mengine, wamesema wakazi.

Karibu watu 5000 walikimbilia katika makanisa. Kwa mujibu wa Padri Silava Sylvain, hali ya kibinadamu inatisha: "Kuna wanawake wasiopungua 500 ambao hutoka asubuhi na mapema kupata mkate, sukari na kahawa.

Vinginevyo kila kitu kimefungwa. Ni vigumu kupata chakula. Ninavyozungumza hapa, hakuna shirika lolote la kutoa msaada ambalo limeshawasili hapa. "

Bouar ni mji wa kimkakati ulioko kwenye barabara muhimu inayotumiwa kwa kuingiza vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula katika mji wa Bangui kutoka Cameroon.