NIGER

Mahamadou Issoufou:Niger imepiga hatua kubwa kidemokrasia

Mahamadou Issoufou,  rais wa Niger
Mahamadou Issoufou, rais wa Niger ©RFI

Rais wa Niger anayeondoka madarakani Mahamadou Issoufou amesema nchi yake inaendelea kuimarika kidemokrasia licha ya kuendelea kushuhudia utovu wa usalama.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii ya rais Issoufou, inakuja wakati huu nchi hiyo inapoendelea kukabiliwa na makundi ya kijihadi yanayosababisha mauaji ya raia na kusababisha malefu ya watu kuyakimbia makwao.

Kiongozi huyo ambaye amekuwa madarakani kwa mihula miwili, anakabidhi madaraka kwa mara ya kwanza katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ndani ya miaka sitini baada ya kupata uhuru wake, hatua ambayo anasema, anajivunia.

Mataifa ya Magharibi hasa Ufaransa iliyokuwa koloni yake, imesifu hatua ya rais Issoufou ya kutobadilisha katiba ili kuendelea kuwa madarakani kama ilivyo kwa viongozi wengine barani Afrika.

Mzunguko wa Uchaguzi wa urais nchini Niger, utafanyika tarehe 21 Februari na mgombea wa chama tawala Mohamed Bazoum, anatarajiwa kupata ushindi dhidi ya mpinzani wake, Mahamane Ousmane.