DRC

Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na kuzorota kwa hali ya usalama Ituri

Maafisa wa usalama wakiwa Ituri, Mashariki mwa DRC
Maafisa wa usalama wakiwa Ituri, Mashariki mwa DRC SAMIR TOUNSI / AFP

Takriban watu 647 wakiwemo wanawake 120 na watoto 115 waliuawa kati ya mwezi Mei na Desemba 2020 na wapiganaji wanaodaiwa kuwa sehemu ya wanamgambo wa kundi la CODECO, kulingana na takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO).

Matangazo ya kibiashara

Mbali na wanamgambo hawa, makundi mengine yenye silaha yameanza kuundwa. Kutokana na kuzorota kwa hali hiyo, UNJHRO na MONUSCO wameomba juhudi zaidi kutoka kwa wadau wote wanaohusika katika kutafuta amani na usalama, ikizingatiwa kuwa mzozo huo unazidi kuwa wa kikabila.

Mnamo mwezi Juni mwaka jana, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alihofia kwamba jamii ambazo zilikuwa wahanga wakuu wa mashambulio ya wanamgambo wa CODECO zinaweza kujifanya kama vikosi vya kujilinda, ikiwa hakutakuwa na ulinzi wa kutosha kutoka vikosi vya usalama na jeshi vya serikali.

Miezi sita baadaye, makundi kadhaa ya wapiganaji yaliundwa, pamoja na wanamgambo wanaojulikana kama "Forces patriotiques intégrationnistes du Congo" (FPIC) na Popular Front for Self-Defense in Ituri (FPAC) / Zaire.

Makundi haya mawili yanaungwa mkono na jamii ambazo kila kundi naonekana kufanya mashambulizi dhidi ya upande mmoja. Kundi la FPIC linaegemea upande wa jamii ya Bira, na kundi la FPAC / Zaire linaegemea upand wa jamii ya Hema.

Hali hiyo ilisababisha vurugu kuenea kutoka maeneo ya Djugu na Mahagi hadi eneo la Irumu.

Katika ripoti yake ya Desemba 2020, kundi la wataalam Umoja wa Mataifa juu ya DRC, lilielezea kuwa ingawa watu wanaounda kundi hili linaloitwa Zaire bado hawajulikani, vyanzo vingi vinabaini kwamba limeundwa na watu wengi kutoka jamii ya Hema na kwamba linaendesha uhalifu wake katika maeneo ya Dala, Mbijo, Mangbwalu na Iga-Barrière, katika eneo la Djugu, huko Berunda, katika eneo la Mahagi, na huko Shari, katika eneo la Irumu.

Kutokana na hali hii, Umoja wa Mataifa umekumbusha tena umuhimu wa kuendelea na kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili, kuanzishwa kwa mpango wa kuaminika wa kupokonya silaha raia wanaozimiliki kinyume cha sheria, kuwarejesha wapiganaji katika maisha ya kiraia, na vile vile kupitishwa kwa sera za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo endelevu.