JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Mahakama yamwidhinisha rais Touadera huku wanajeshi wengine wa Kimataifa wakiuawa

Mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati FLORENT VERGNES / AFP

Waasi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamewauwa wanajeshi wengine wawili wa Umoja wa Mataifa MINUSCA, na kufikisha idadi ya wanajeshi saba waliouwa katika siku za hivi karibuni kutokana na makabiliano yanaoendelea nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya Umoja wa Mataifa, imesema wanajeshi waliouwa ni kutoka nchini Gabon na Morocco, na walishambuliwa walipokuwa kwenye gari lao karibu na mji wa Bangassou, ambao vikosi vya MINUSCA vinasema vilidhibiti mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mauaji haya ya hivi punde yamekuja baada ya Mahakama nchini humo kuthibitisha kuwa rais Faustin Archange Touadera alishinda Uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Desemba mwaka uliopita.

Rais wa Jamhuri ya Kati  Faustin-Archange Toudéra.
Rais wa Jamhuri ya Kati Faustin-Archange Toudéra. Ludovic MARIN / AFP

Jaji wa Mahakama ya Katiba, Daniele Darlan alisema Touadera alishinda uchaguzi huo katika mzunguko wa kwanza kwa kupata asilimia 53.16 ya kura na kumshinda Waziri Mkuu wa zamani Anicet Georges Dologuele aliyepata asilimia 21.69.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, rais Touadera ameomba mshikamano nchini humo.

‘Nawaomba wazalendo wote, tuungane pamoja na kuiepusha  nchi yetu kwenye mizozo na utovu wa usalama,” alisema.

Touadera mwenye umri wa miaka 63, amekuwa akiongoza taifa hilo tangu mwaka 2016.