DRC

Mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi CENI Ngoyi Mulunda akamatwa

Mchungaji Daniel Ngoy Mulunda, mwenyekiti wa zamani tume ya uchaguzi CENI nchini DRC.
Mchungaji Daniel Ngoy Mulunda, mwenyekiti wa zamani tume ya uchaguzi CENI nchini DRC. RFI/Bruno Minas

Aliyekuwa mwenyekiti  wa tume ya uchaguzi CENI nchini DRC, mchungaji Ngoyi Mulunda anashikiliwa na vyombo vya usalama kwenye mji mkuu wa mkowa wa haut Katanga, Lubumbashi baada ya kushutumiwa kuwa alitumia lugha za uchochezi wakati wa kusomwa misa ya kumkumbuka rais aliyeongoza kile kinachoitwa ukombozi wa taifa hilo, marehemu Laurent Kabila aliyeuawa ofisini kwake Januari 16 mwaka 2001 jijini Kinshasa.

Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya habari mjini Lubumbashi vimeripoti kuwa mchungaji Ngoyi Mulunda alikamatwa saa za alasiri mwanzoni mwa juma hili, punde baada ya kumalizika kwa misa kubwa iliyowakusanya maelfu ya wananchi katika kanisa lake ambapo wananchi pamoja na wanasiasa waliomkumbuka rais Laurent Desire Kabila aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake akiwa ofisini mwaka 2001.

Miaka 20 sasa imepita kesi ya mauaji ya Laurent Kabila, mtu aliyechukuliwa kama mkombozi wa pili wa taifa hilo baada ya kuuangusha utawala wake Mobutu Sese Seko Kuku Ngbwendu wa Za Banga.

Kesi ya mauaji yake bado imekuwa ikisuasua, licha ya hivi karibuni mtu aliyedaiwa kuwa mhusika kwa njia moja ama nyingine wa mauaji hayo, kanali Eddy Kapend kuachiwa huru pamoja na washirika wengine ishirini, na amabo waliachwa huru kufwatia msamaha wa rais wa sasa Felix Tshisekedi.

Taarifa zinasema mchungaji Mulunda alitumia lugha mbaya inayoweza kuzusha uhasama kati ya watu wa Katanga na wazawa wa mkowa wa Kasai anakotoka rais wa sasa, Tshisekedi huku Kabila akichukuliwa kuwa mzaliwa wa Katanga.

Kukamatwa kwake kumezua mvutano mkubwa siku ya jumanne alasiri ambapo wafuasi wa mchungaji huyo wamekabiliana na waendesha bodaboda maarufu wewa kwenye mji wa Lubumbashi. Maafisa wa usalama hawajaeleza idadi ya vifo wala majeruhi yaliyosababishwa na vurugu hizo.