TANZANIA-UINGEREZA

Uingereza yazuia raia wa Tanzania na DRC kuingia nchini mwake kwa hofu ya virusi vipya vya Covid 19

Picha ya maktaba ya rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Picha ya maktaba ya rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli. REUTERS/Thomas Mukoya/File Photo

Serikali ya Uingereza, imeweka marufuku ya kuingia nchini humo raia kutoka katika mataifa ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuanzia Ijumaa tarehe 22 kama njia ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vipya vya Corona ambavyo asili yake ni nchini Afrika Kusini.  

Matangazo ya kibiashara

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter, waziri wa masuala ya usafiri, Grant Shapps, amesema "Wasafiri wote kutoka kwenye nchi hizi isipokuwa raia wa Uingereza na jamhuri ya Ireland na zile za dunia ya tatu ambao wana haki ya kuishi nchini humo hawataruhusiwa kuingia".

"Tunaendelea kufuatilia mwenendo wa maambukizi ya virusi hivi kwa lengo la kuhakikisha tunalinda mipaka yetu kwa watu wanaoingia na kutoka". alisema waziri Grant Shapps.

Mwanzoni mwa mwaka huu Serikali ya Uingereza ilitangaza kuwazuia kuingia nchini humo raia kutoka katika mataifa takribani 11 ya kusini mwa Afrika kwa sababu ya kudhibiti maambukizi mapya.

Juma hili kituo cha Afrika cha udhibiti wa magonjwa CDC, kilisema maambukizi ya Covid 19 barani Afrika sasa yako kwa kiwango cha juu kwa asilimia 2.5 tofauti kabisa na kiwango cha dunia cha sasa cha asilimia 2.2.

CDC iliiorodhesha nchi ya DRC kama miongoni m^wa mataifa 21 ya Afrika ambayo maambukizi yake yako kwa asilimia zaidi ya 3.

Tangu mwaka jana nchi ya Tanzania ilitangaza kuwa huru na virusi vya corona, huku kukiwa hakuna takwimu zozote rasmi zikionesha mwenendo wa maambukizi nchini humo.

Hatua ya Tanzania kutotoa taarifa za mwenendo wa ugonjwa huo, ulikosolewa vikali na shirika la afya duniani WHO pamoja na mataifa kadhaa ya magharibi ambayo yametaka raia wake kuchukua tahadhari pindi wanapotembelea taifa hilo.

Mamlaka za Tanzania na DRC bado hazijatoa taarifa yoyote kuhusu katazo hilo la Serikali ya Uingereza.