SAHEL

Watu milioni mbili walazimika kuyahama makaazi yao Sahel

Mwanajeshi wa Ufaransa katika eneo la Sahel lenye makundi ya kijihadi
Mwanajeshi wa Ufaransa katika eneo la Sahel lenye makundi ya kijihadi AFP Photo/MICHELE CATTANI

Shirika la umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR) limetoa wito wa kukomeshwa kwa "ghasia zisizokoma" huko Sahel, "ambazo zimesababisha zaidi ya watu milioni mbili kuyahama makaazi yao kila mara.

Matangazo ya kibiashara

Idadi hiyo, ikiwa ni kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kulingana na Umoja wa Mataifa, inaripotiwa nchini Burkina Faso, Chad, Mali na Niger .

Kulingana na Umoja wa Mataifa idadi hiyo "imeongezeka mara nne katika miaka miwili tu", kwani idadi ya wakimbizi wa ndani ilikua 490,000 mwanzoni mwa mwaka 2019. Zaidi ya nusu ya wakimbizi wa ndani katika eneo hilo ni kutoka Burkina Faso.

Tayari watu 21,000 wako mafichoni tangu mapema mwezi Januari

Tangu kuanza kwa mwaka huu pekee, vurugu nchini Niger na Burkina Faso zimesababisha zaidi ya watu 21,000 kukimbia makazi yao na kukimbilia katika maeneo ya nchi jirani, kulingana na UNHCR.

Nchini Burkina Faso mashambulizi ya makundi yenye silaha dhidi ya mji wa Koumbri na vijiji  jirani kaskazini mwa nchi yamesababisha zaidi ya watu 11,000 kuyatoroka makaazi yao. Wengi wao ni wanawake na watoto waliokimbia usiku baada ya washambuliaji kuanza kufyatua risasi kwenye nyumna zao.