GHANA

Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings kuzikwa Jumatano Januari 27

Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings.
Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings. REUTERS

Miezi mitatu baada ya kifo cha rais wa zamani wa Ghana,  Jerry Rawlings mnamo Novemba 12, 2020 huko Accra, taratibu za mazishi yake zimeanza tangu Jumapili Januari 24 katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Jana Jumapili alasiri kulifanyika ibada ya misa ya uzinduzi ambayo ilifungua shughuli ya mazishi ya serikali ya Jerry Rawlings.

Familia ya marehemu ilikuwa mstari wa mbele, pamoja na rais Nana Akufo-Addo na kiongozi wa chama cha upinzani John Mahama, kuhudhuria mahubiri yaliyotolewa na Askofu Mkuu wa Cape Coast.

Shughuli hiyo iliendelea jana jioni katika makao makuu ya jeshi la Anga. Jerry Rawlings alikuwa rubani wa ndege za kijeshi kabla ya kuchukua madaraka mnamo mwaka 1981.

Zoezi la kuuaga mwili wa hayati rais Jerry Rawlings litafanyika Jumatatu na Jumanne wiki hii katika mji mkuu. Wajumbe wa serikali watapishana katika Jumba la Burning kwa heshima ya mwisho kwa mkuu wa zamani wa nchi. Sehemu zingine pia zitakuwa wazi kwa umma.

Wakuu wa jadi wa eneo la Anlo, alikotokea Rawlings, wiki hii iliyopita walitaka mwili wake kurudishwa katika mkoa wao mashariki mwa nchi. Walitarajia kumzika rais huyo wa zamani katika mkoa huo kulingana na ibada zao za mazishi. Ombi lao halitazingatiwa.

Sherehe za mazishi zitafanyika Jumatano katika Uwanja wa Uhuru, na Jerry Rawlings atazikwa katika makaburi ya jeshi la Accra, kama wakuu wa nchi waliomtangulia.