MALI

CNSP yavunjwa, rais N'Daw apokelewa Élysée

Waziri Mkuu wa Mali Moctar Ouane
Waziri Mkuu wa Mali Moctar Ouane RAVEENDRAN / AFP

Kamati ya Kitaifa ya Wokovu kwa Watu (CNSP), chombo kilichoundwa na kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali mnamo Agosti 18 2020, imevunjwa rasmi.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni kwa mujibu wa sheria iliyotiwa saini hasa na rais wa mpito na Waziri Mkuu Moctar Ouane.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ilikuwa imehimiza hivi karibuni kufutwa kwa chombo hiki ambacho kilikuwa kikiendelea kuimarisha utawala wa kijeshi nchini Mali.

Hata kama kufutwa kwa chombo hiki ni tukio kubwa, wanajeshi bado wana ushawishi mkubwa nchini humo.

CNSP sasa imefutwa rasmi, lakini maafisa wake wakuu wa jeshi hawajarudi kwenye kambi na wanaendelea kuripoti kazini.

Kwa mfano, rais wa zamani wa CNSP, Kanali Assimi Goïta, tayari anashikilia wadhifa wa makamu wa rais wa mpito, ndiye kiongozi namba 2 wa serikali. Makamu mwenyekiti wa zamani wa kamati iliyofutwa, Kanali Malick Diaw, ni mkuu wa Baraza la Mpito la Kitaifa, chombo kinachotunga sheria. Vigogo wengine wakubwa katika kundi hili lililofanya mapinduzi wana nyadhifa kubwa serikalini.

Jeshi kukabidhi madaraka kwa raia bado ni ndoto nchini Mali, wakati jeshi hilo linaendelea kudai kwamba linashikilia baadhi ya nyadhifa katika serikali kukabiliana na makundi ya wanamgambo wa kiislamu.