DRC-SIASA

Waziri Mkuu wa DRC Sylvestre Ilunga Ilunkamba ajiuzulu

Aliyekuwa Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba.
Aliyekuwa Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba. Présidence de la République démocratique du Congo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Sylvestre Ilunga Ilunkamba, amejiuzulu siku ya Ijumaa, siku mbili baada ya wabunge kupiga kura ya kukosa imani naye.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inampa nafasi rais Felix Thisekedi kuunda serikali mpya, itakayoongozwa na Waziri Mkuu mpya ambaye atakuwa ni mshirika wake wa karibu baada ya kupata wingi wa wabunge.

Msemaji wa rais Giscard Kusema amesema Ilunga amefikia hatua hiyo kwa kuheshimu uamuzi wa wabunge na mazingira ya kisiasa nchini humo.

Ilunga, mshirika wa karibu wa rais wa zamani Joseph Kabila, alitakiwa kujiuzulu kikatiba baada ya wabunge kukosa imani naye.

Rais Thisekedi, ambaye tayari amepata wingi wa wabunge bungeni ambao ni 391 kati ya 500, sasa anasubiriwa kutangaza serikali mpya katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Awali, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 73 kupitia ukurasa wake wa Twitter, aliandika kuwa yupo tayari kuachia madaraka baada ya uamuzi wa wabunge nchini humo.