ALGERIA

Algeria yavunja Bunge, uchaguzi wa mapema waitishwa

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune France 24

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune ametangaza kulivunja Baraza la Wawakilishi na kuitisha uchaguzi wa mapema.

Matangazo ya kibiashara

Abdelmadjid Tebboune ametangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri katika muda wa saa 48 zijazo wakati wa hotuba ya televisheni Alhamisi usiku.

"Nimeamua kuvunja Baraza la Wawakilishi na kuitisha uchaguzi mpya ili kuweka taasisi mpya", alitangaza bila hata hivyo kutoa tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Wajumbe wa Baraza la wawakilishi walichaguliwa mnamo mwaka 2017, wakati washirika wa Abdelaziz Bouteflika, mtangulizi wa Abdelmadjid Tebboune, walikuwa wengi katika baraza hilo.

Abdelmadjid Tebboune amesema uamuzi huo ni sehemu ya mageuzi yenye lengo la kutoa nguvu zaidi kwa bunge.

Katika hali ya kutuliza mvutano wa kisiasa rais Abdelmadjid Tebboune ametoa msamaha kwa wanaharakati zaidi ya hamsini wa vuguvugu la Hirak. Hatua hii inawahusu hasa watu karibu 30 waliohukumiwa mapema wiki hii kifungo cha hadi miaka 2 jela.

Rais wa Algeria hajataja majina, lakini ameahidi kwamba "kati ya watu 55 na 60 watajiunga na familia zao kuanzia kesho". Hatua hii inakuja siku chache kabla ya maadhimisho ya pili ya kuanzishwa kwa vuguvugu la Hirak.