LIBYA- UN

Mwanzilishi wa kampuni ya Blackwater atuhumiwa kukiuka vikwazo vya silaha Libya

Wakimbizi kutoka Libya wakikimbilia eneo la fukwe za Libya kutafuta hifadhi kwenye mataifa ya Ulaya
Wakimbizi kutoka Libya wakikimbilia eneo la fukwe za Libya kutafuta hifadhi kwenye mataifa ya Ulaya REUTERS/Ismail Zitouny

Erik Prince, mshirika wa karibu wa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump na mwanzilishi wa kampuni ya usalama ya kibinafsi ya Blackwater, alikiuka vikwazo vya silaha nchini Libya. Habari hiyo imefichuliwa na magazeti ya New York Times na Washington Post, ambayo waliweza kupata ripoti ya kurasa 121 kutoka Umoja wa Mataifa.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na ripoti hiyo ya siri kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Erik Prince alituma mamluki wa kigeni nchini Libya, vifaa vya vifaa vya kijeshi, boti, helikopta na ndege tatu kutoka Jordan.

Ni operesheni ya kiasi cha dola milioni 80 ambazo Erik Prince aliweza kutumia mnamo mwezi Julai 2019. Lengo la operesheni hii ilikuwa kumsaidia Khalifa Haftar, mbabe wa kivita Mashariki mwa Libya, katika jaribio lake la kuiangusha serikali ya Libya inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa mnamo mwaka 2019, ikiwa ni pamoja na kutekeleza mauaji dhidi ya maafisa wakuu wa Libya.

Magazeti ya New York Times na Washington Post yalipata ripoti hii ya kurasa 121 iliyoandaliwa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kulingana na ripoti hii, Erik Prince alituma mamluki wa kigeni na silaha kwa Khalifa Haftar.

Kulingana na wakili wake, Erik Prince hana "uhusiano wowote na operesheni ya Libya ya mwaka 2019". Ikiwa alikuwa mshirika wa karibu wa rais wa zamani Donald Trump, mwanzilishi wa Blackwater hawezi kupata uungwaji mkono kutoka White House.

Erik Prince, ambaye pia ni kaka wa Waziri wa zamani wa Elimu Betsy DeVos, ni mwanzilishi wa kampuni ya usalama ya kibinafsi ya Blackwater, ambapo maafisa wake wanne wa zamani walihukumiwa kwa mauaji ya raia 14 wa Iraq mnamo mwaka 2007, katika mji wa nchi hiyo Baghdad, lakini walisamehewa na Donald Trump mnamo mwezi Desemba 2020.

Anaweza kukabiliwa na vikwazo kutoka Umoja wa Mataifa na huenda akaunti zake za benki zikazuiliwa na vile vile kuzuiwa kusafiri nje ya nchi.

Libya iko chini ya vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2011 kwa matumizi ya vurugu dhidi ya raia.