NIGER- SIASA

Zoezi la uhesabuji kura laendelea Niger

Mfanyakazi wa tume ya uchaguzi nchini Niger jumapili akiandaa masanduku ya kupigia kura mjini Niger Febuary 20, 2021.
Mfanyakazi wa tume ya uchaguzi nchini Niger jumapili akiandaa masanduku ya kupigia kura mjini Niger Febuary 20, 2021. Issouf Sanago / AFP

Wananchi wa Niger, wanasubiri mshindi wa mzunguko wa pili wa uchaguzi wa urais, baada ya kupiga kura hapo jana, zoezi ambalo lilishuhudia vifo vya maafisa saba wa tume ya Uchaguzi walioshambuliwa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa aradhini katika jimbo la Tillaberi. 

Matangazo ya kibiashara

Wapiga kura milioni 7.5 wa Niger walipiga kura Jumapili Februari 21 ikiwa ni duru ya pili ya uchaguzi wa urais kati ya mgombea wa chama tawala cha PNDS  Mohamed Bazoum (ambaye alichukuwa nafasi ya kwanza katika duru ya kwanza kwa 39% ya kura), na mgombea wa upinzani wa chama cha RDR Tchanji Mahamane Ousmane (aliyechukuwa nafasi ya pili akipata karibu 17%).

Uchaguzi huo kwa ujumla ulifanyika katika mazingira mazuri, ingawa vifo kadhaa viliripotiwa katika jimbo laTillabéri.

Katika eneo hilo lisilo salama, maafisa saba wa tume ya uchaguzi walipoteza maisha baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini Jumapili asubuhi katika eneo linalopatikana katika wilaya ya Dargol, katika eneo la mipaka mitatu.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger Alkache Alhada amewaambia waandishi wahabari kuwa zoezi la kupiga kura halikufanyika katika vituo kadhaa vya kupigia kura kutokana na tukio hilo, ambapo serikali yake ilianza kuchukua hatua za kiusalama ili uchaguzi huu ufanyike katika mazingira mazuri zaidi.

Wakati huo huo tume ya uchaguzi CENI ilibaini kwamba iligundua kadi za kupigia kura za uwongo katika manispaa ya mikoa ya Dosso na Agadez.