DRC- USALAMA

Mwili wa balozi wa Italia Luca Attanasio aliyeuawa mashariki mwa DRC wawasili nyumbani

Jeneza linalobeba mwili wa balozi wa aliyeuawa mashariki mwa DRC February 24 2021
Jeneza linalobeba mwili wa balozi wa aliyeuawa mashariki mwa DRC February 24 2021 AP - Justin Kabumba

Mwili wa balozi wa Italia Luca Attanasio, aliyeuawa mwanzoni mwa juma hili mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, baada ya kushambuliwa na waasi katika maeneo ya Kibumba nje kidogo ya jiji kuu la Goma, umerudishwa nyumbani leo mjini Roma, na kupokelewa na Waziri Mkuu Mario Draghi.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Kinshasa imewashutumu waasi wa kihutu wa FDLR tawi linalofahamika kama FDLR/FOCA kuhusika na kifo cha balozi huyo jumatatu ya february 22.

Hata hivyo, msemaji wa kundi hilo kanali Placide Niyiturinda ameyakanusha madai ya serikali huku akisema kuwa wapiganaji wao wameweka ngombe zao katika maeneo yaliyo mbali na eneo la tukio hilo.

Wakati akijibu maswali ya wabunge hivi leo kuhusu kifo cha balozi Attanasio, waziri wa mambo ya nje wa Italia Luigi Di Maio amesema kuwa amelitaka shirika la mpango wa chakula duniani WFP pamoja na umoja wa mataifa kufanya uchunguzi juu ya shambulio lililogharimu maisha ya balozi Attanasio nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Di Maio amesema serikali yake imeitaka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kueleza kuhusu mipango ya kiusalama ilivyoshughulikiwa tangu balozi Luca alipoondoka jijini Kinshasa kuelekea eneo la mashariki mwa nchi hiyo, kabla ya kuuawa kwake yeye, mlinzi wake ambaye  pia ni raia wa Italia pamoja na dereva wao ambaye ni raia wa DRCongo.