NIGER-UCHAGUZI-SIASA

Niger: Bazoum atangazwa mshindi, upinzani wapinga

Mgombea wa chama tawala Niger Mohamed Bazoum akisalimiana na wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais huko Niamey, Niger Februari 23, 2021.
Mgombea wa chama tawala Niger Mohamed Bazoum akisalimiana na wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais huko Niamey, Niger Februari 23, 2021. REUTERS - STRINGER

Mgombea wa chama tawala katika uchaguzi wa urais nchini Niger, Mohamed Bazoum, ameibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa asilimia 55.75 ya kura dhidi ya mgombea wa upinzani Mahamane Ousmane (44.25%), Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi imetangaza.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo yaliyotagazwa bado ni "ya muda", amesema mwenyekiti wa CENI, Issaka Souna.

Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi ilitangaza, Jumanne alasiri, matokeo ya jumla ya muda ya duru ya pili ya uchaguzi huu wa urais, wakati wa hafla fupi katika majengo ya makao makuu ya Baraza la Wawakilishijijini Niamey.

Kulingana na takwimu hizi, mgombea wa chama tawala cha PNDS, Mohamed Bazoum, anaongoza kwa asilimia 55.75 ya kura. Mpinzani wake Mahamane Ousmane, mgombea wa chama cha RDR Tchanji, amepata 44.25% ya kura zilizopigwa. Na kulingana na matokeo haya yaliyotangazwa na CENI, kiwango cha ushiriki kilifikia 62.91%.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Issaka Souna, alisema matokeo hayo ni ya muda na yatachunguzwa na Mahakama ya Katiba.

Wakati huo huo upinzani umefutilia mbali matokeo hayo, ukibaini kwamba uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa.