CONGO BRAZZAVILLE- UCHAGUZI

Congo Brazzaville: Asasi za kiraia zashuku Mpango wa kuandaa udanganyifu wa kura

Chama tawala nchini Congo Brazzaville chamteua Denis Sassou-Nguesso kama mgombea urais wa 2021.
Chama tawala nchini Congo Brazzaville chamteua Denis Sassou-Nguesso kama mgombea urais wa 2021. AFP PHOTO / THIERRY CHARLIER

Asasi mbili za kiraia nchini Congo Brazzavile Jumatano Februari 24 zimedhihirisha wasiwasi wao kuhusu kile kinachoelezwa kusukwa kwa mipango mikakati ya kufanyika kwa udanganyifu wa kura katika chaguzi zinazopangwa kufanyika tarehe 21 mwezi machi mwaka huu, ambapo rais anayemaliza muda wake Denis Sassou Nguesso anagombea tena pamoja na wagombea wengine sita.

Matangazo ya kibiashara

Awali maaskofu wa kanisa katoliki walishutumu tume ya kitaifa ya uchaguzi kwenye nchi hiyo kwa kudhihirisha ukimya baada ya rais wa nchi hiyo Denis Sassou Nguesso kuanzisha kampeni za mapema mwezi uliopita kwa kuzinduwa bwawa la umeme na maeneo mengine.

Kwa upande wake shirika la haki za binaadamu kwa ajili ya maendeleo nchini humo linalofahamika kama CDHD pamoja na Harakati ya wananchi maarufu, Ras-le-Bol yameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya mchakato mzima wa uchaguzi huku yakishuku kwamba huenda uchaguzi wa mwezi marchi usiwe huru na haki.

Mwenyekiti wa shirika la haki za binaadamu kwa ajili ya maendeleo nchini humo la CDHD, Roch Euloge Nzobo licha ya kukiri kufanyika kwa baadhi ya marekebisho katika baadhi ya orodha za wapiga kura, ameenda mbali na kusema kuwa tume ya uchaguzi nchini wala serikali haijakubali kufanyiwa marekebisho orodha ya wapigakura, wala mabadiliko ya uongozi wa tume hiyo kama ilivyoainishwa katika sheria za uchaguzi nchini humo.  

Wawakilishi wa asasi hizo mbili wanasema idadi ya wapiga kura bado haijulikani.