DRC-USALAMA

Saba wauawa na wanamgambo wa CODECO huko Banyari Kilo, DRC

Kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, katika mji wa Djugu.
Kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, katika mji wa Djugu. © Samir Tounsi / AFP

Watu saba wameuawa kaskazini mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wakati wa shambulio lililodaiwa kuwa lilitekelezwa na wanamgambo wa CODECO katika vijiji vya Tchibi Tchibi, K25 Mongali na Kabakaba, katika sekta ya Banyari Kilo, wilayani Djugu katika mkoa wa Ituri, kulingana na ripoti ya mashirika ya kiraia.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti hiyo ya mashirika ya kiraia katika eneo hilo inasema mashambulizi hayo yalifanyika siku mbili zilizopita, Jumanne ya Februari 23 na Jumatano Februari 24, licha ya jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuingilia kati katika eneo la Djugu (Ituri).

Miongoni mwa watu waliouawa ni pamoja na vijana wanne ambao waliuawa kikatili wakati wapiganaji hao wa CODECO walipokuja  kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya mwanamke mmoja na wachimbaji  wawili wa dhahabu ambao walipigwa risasi na kufa katika eneo lenye madini ya dhahabu.

Tangu jeshi la nchi hiyo kuanzisha mashambulio yanayolenga kulitokomeza kundi hilo la uasi huko Mongwalu, kumekuwa na mfululizo wa mauaji na mashambilizi ya kuvizia dfhidi ya raia wa kawaida kwenye mkoa huo wa Ituri.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya vijana amefahamisha kuwa wanamgambo watatu waliofaulu kukimbia, waliwafyatulia risasi wachimba dhahabu kwenye machimbo yanayojulikana kama "Amerika" katika kijiji cha Kabakaba, ambapo wachimbaji watatu wa dhahabu walikufa na mwingine alijeruhiwa, na kuongeza kuwa wanamgambo hawa walimbaka mwanamke mmoja, naye amelazwa katika kituo cha afya huko Itendey.