CAR-ICGLR-USALAMA

Mkutano wa Luanda kuhusu Jamhuri ya Afrika ya Kati waahirishwa

Faustin Archange Touadéra rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Faustin Archange Touadéra rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. REUTERS/Sergei Karpukhin

Jeshi na washirika wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaendelea na operesheni ya kudhibiti maeneo muhimu nchini humo yanayoshikiliwa na waasi.

Matangazo ya kibiashara

Wiki hii jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati lilidhibiti mji wa Bossangoa. Na Jumamosi hii mkutano wa kilele chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR) ulikuwa ufunguliwe katika mji mkuu wa Angola, Luanda, lakini umehirishwa kwa mara ya pili bila maelezo zaidi.

Jumuiya ya Kanda ya Maziwa Makuu ilitarajia kuandaa mkutano kwa lengo la kuendeleza mazungumzo ili kumaliza ghasia zinazoendelea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu katikati ya mwezi wa Desemba. Lakini maandamano kadhaa yamefanyika katika jiji la Bangui na mbele ya makao makuu ya ECCAS katika wiki za hivi karibuni kupinga mazungumzo na waasi.

Kuhusu suala hilo,ikulu ya rais jijini Bangui ilitoa msimamo wake jana Ijumaa. Ikiwa rais Faustin Archange Touadéra atafanya ziara katika mji mkuu wa Angola, Luanda, itakuwa kubaini msimamo wake: hakutakuwa na mazungumzo na wale ambao hawaheshimu masharti ya makubaliano ya amani. Hawa "lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani," amesema msemaji wa ikulu ya rais.

Wakati huo huo, Baraza la Uchumi na Jamii la Jamhuri ya Afrika ya Kati lilipokea wawakilishi wa vyama vya kiraia na vyama vya siasa vya upinzani kwa lengo la mazungumzo ya kitaifa. Ripoti ya hitimisho la mashauriano haya itawasilishwa kwa mamlaka. Ikulu ya rais imebaini kwamba  mchakato wa uchaguzi lazima kwanza umalizike ili kufikiria kufungua mpango huo.