NIGERIA-USALAMA

Mamia ya wasichana waliotekwa nyara nchini Nigeria waachiliwa huru

Mamia ya wasichana wa waliotekwa nyara wiki iliyopita katika shule yao ya bweni huko Jangebe, wameachiliwa.
Mamia ya wasichana wa waliotekwa nyara wiki iliyopita katika shule yao ya bweni huko Jangebe, wameachiliwa. REUTERS - AFOLABI SOTUNDE

Mamia ya wasichana wa waliotekwa nyara Ijumaa ya wiki iliyopita katika shule yao ya bweni huko Jangebe kaskazini magharibi mwa Nigeria wameachiliwa huru na wako Jumanne hii asubuhi katika majengo ya serikali ya Zamfara, gavana wa jimbo hilo Dkt Bello Matawalle ameliambia shirika la habari la AFP.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na waandishi habari, Matawalle amesema kuwa jana maafisa wa serikali walifanya mazungumzo na watekaji nyara na kwamba hawakuwa na nia ya kupeleka vikosi vya usalama kwa hofu ya kuyaweka hatarini maisha ya wasichana hao.

"Mungu asifiwe! Nina furaha kutangaza kuachiliwa kwa wanafunzi waliotekwa nyara katika shule ya Upili ya GGSS Jangebe," ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

"Jumla ya wasichana waliotekwa nyara katika shule hiyo ni 279, wote wako hapa nasi, tunamshukuru Mwenyezi Mungu," gavana huyo ameongeza.

Awali viongozi walidai kuwa wasichana  317 walikosekana baada ya shambulio dhidi ya shule hiyo ya bweni katika jimbo la Zamfara usiku wa Alhamisi kuamkia Ijumaa. Shambulio lililotekelezwa na kundi la watu wenye silaha.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP ameona mamia ya wasichana, wakiwa wamevalia hijabu za rangi ya samawati, wakiwa wamekusanyika katika jengo la serikali

Hili ni shambulio la nne dhidi ya shule chini ya kipindi cha miezi mitatu Kaskazini Magharibi mwa Nigeria, ambapo makundi ya wahalifu vyanayojulikana kama "majambazi" yamekuwa yakifanya uvamizi mkubwa wa ng'ombe na kuteka nyara yakiomba fidia kwa zaidi ya miaka kumi.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amesema amepokea kwa furaha taarifa za kuachiliwa huru wasichana hao na kwamba anaungana na familia zao na watu wote wa Zamfara kusherehekea ushindi huo. Rais Buhari ametoa wito wa kuwepo umakini zaidi kwa ajili ya kuwazuia wahalifu kufanya mashambulizi mengine kama hayo na ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya watekaji.